1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky: 2023 utakuwa mwaka wa ushindi kwa Ukraine

30 Januari 2023

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema ana uhakika nchi yake inaweza kuishinda Urusi mwaka huu, licha ya changamoto wanayokumbana nayo katika uwanja wa mapambano.

Ukraine Soledar Wagner Söldner
Picha: SNA/IMAGO

Akilituhubia taifa usiku wa kuamkia Jumatatu, Zelensky amekiri kuwa hali bado ni ngumu, kutokana na mapigano makali mashariki mwa nchi hiyo. ''Hali katika eneo la mapambano ni mbaya, hasa kwenye jimbo la Donetsk na maeneo ya kusini. Miji ya Bakhmut, Vuhledar na maeneo mengine katika jimbo la mashariki la Donetsk, inaendelea kushambuliwa kwa makombora ya kila mara ya Urusi,'' alisisitiza Zelensky

Ukraine inahitaji haraka silaha mpya

Zelensky amesema Ukraine inahitaji haraka silaha mpya ili kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi ya Urusi huko Donetsk. Amewatolea wito washirika wake kuongeza kasi ya upelekaji wa silaha, akisisitiza kuwa hali nchini mwake bado ni mbaya. Zelensky amesema Urusi inataka vita viendelee na inajaribu kuvidhoofisha vikosi vya Ukraine.

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema nchi yake haitopeleka Ukraine ndege za kivita. Ukraine iliomba kupatiwa ndege za kivita, baada ya Ujerumani kukubali kuipatia nchi hiyo vifaru vya kivita chapa Leopard 2. Katika mahojiano yake na gazeti la Tagesspiegel, Scholz ameonya kuhusu hatari ya kuongeza mvutano, wakati ambapo Urusi tayari imelaani vikali ahadi ya kupelekwa vifaru hivyo.

Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Ryabkov amesema Jumatatu kuwa baada ya Marekani kuamua kuipatia vifaru Ukraine, hakuna haja ya Urusi kuzungumza na Ukraine au washirika wake wa Magharibi. Ryabkov amesema hakuna mtu katika nchi za Magharibi ambaye amekuja na mipango yoyote madhubuti ya kuutatua mzozo wa Ukraine.

Watu watatu wauawa Kherson

Aidha, Rais Zelensky amesema watu wapatao watatu wameuawa katika mji wa Kherson siku ya Jumapili na wengine sita wamejeruhiwa katika shambulizi la kombora la Urusi, na mwingine mmoja ameuawa katika shambulizi kwenye mji wa Kharkiv. Watu wanne pia wameuawa katika mkoa wa Zaporizhzhia, ambako mapambano yalipamba moto katika siku za hivi karibuni.

Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson amesema kwamba Rais wa Urusi Vladmir Putin, alimtishia kwa shambulizi la kombora muda mfupi kabla ya kuivamia Ukraine.

Johnson ameyasema hayo katika kipindi cha Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC kinachotarajiwa kurushwa Jumatatu. ''Kwa namna fulani alinitishia wakati mmoja na kusema,'' Boris sitaki kukuumiza, lakini kwa shambulizi la kombora itachukua dakika moja tu, au kitu kama hicho,'' alifafanua Boris.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris JohnsonPicha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg ameitolea wito Korea Kusini kuongeza msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine. Akizungumza Jumatatu mjini Seoul, Stoltenberg amezitolea mfano nchi ambazo zimebadili sera yao ya kutotoa silaha kwa nchi zilizoko kwenye mizozo baada ya uvamizi wa Urusi.

Stoltenberg yuko Seoul katika kituo cha kwanza cha ziara yake ambayo itaijumuisha pia Japan, yenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya muungano huo wa kijeshi na washirika wa Marekani katika kukabiliana na vita vya nchini Ukraine na kuongezeka kwa ushindani na China.

Na katika michezo Zelensky amewataka wanariadha wa Urusi waondolewe kwenye michezo ya Olympic iliyopangwa kufanyika Paris Ufaransa mwaka 2024. Amesema kuiruhusu Urusi kushiriki ni sawa na kuonesha kuwa ugaidi unakubalika kwa kiwango fulani.

(DPA, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW