1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aapa kuikomboa Crimea kutoka mikononi mwa Urusi

Saleh Mwanamilongo
23 Agosti 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameapa kulirejesha jimbo lililonyakuliwa na Urusi la Crimea chini ya utawala wa Ukraine.

Ukraine-Krieg | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Ukraine Presidential Press Service/AFP

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika kwa njia ya vidio, Zelensky amesema uchokozi wa Urusi ulianza na jimbo la Crimea na utamalizika na jimbo hilo. Mkutano huo unalenga kurejesha uadilifu wa eneo nzima la Ukraine na kukomesha uvamizi wa Urusi kwenye eneo la Crimea.

"Na hii ni kweli, na ninaamini kwa asimilia mia moja kwamba kuushinda ugaidi, kurudisha dhamana na usalama kwenye kanda yetu, kwa Ulaya, kwa ulimwengu wote, ni muhimu kupata ushindi katika vita dhidi ya uvamizi wa Urusi.",asema Zelensky.

Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi aliuambia mkutano huo kwamba nchi yake itaendelea kuiunga mkono Ukraine. Draghi amesema Roma iko pamoja na Zelensky katika nafasi yake ya kupigana kupinga uvamizi wa Urusi, kulinda demokrasia na uhuru wa Ukraine.

Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitoa wito wa nchi za magharibi kutokuwa na udhaifu mbele ya Urusi, akiitaka kwa mara nyingine tena Moscow kusitisha mapigano,na kuondoa wanajeshi wake katika ardhi yote ya Ukraine.

Miongoni mwa wanao hudhuria mkutano huo ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg. Jumla ya washiriki 50 kutoka pande zote za dunia walioalikwa wameshiriki.

Poland yaahidi msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Rais wa Poland Andrzej Duda (kushoto) mjini Kyiv kujadili msaada zaidi kwa UkrainePicha: Ruslan Kaniuka/Ukrinform/ABACA/picture alliance

Rais wa Poland Andrzej Duda amesafiri kwenda Kiev kukutana na Rais wa Ukraine Zelensky kujadili msaada wa kijeshi na kibinadamu.

Mamlaka nchini Ukraine imepiga marufuku sherehe za umma katika mji mkuu wa Kyiv wakati wa maadhimisho ya miaka 31 ya uhuru wa Ukraine kutoka utawala wa Kisovieti kesho Jumatano, ikitoa sababu za kuwepo kwa tishio kubwa la usalama.

Chanzo kingine cha wasiwasi kwa jumuiya ya kimataifa ni hatma ya wafungwa wa vita wa Ukraine. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet alielezea

wasiwasi wake kuhusu ripoti kwamba Urusi na vikundi vya wapiganaji vinavyoiunga mkono huko Donetsk wanapanga kuwahukumu wafungwa hao.

Hata hivyo, mbali na taarifa za vifo na uharibifu, la kutia moyo nchini humo ni kuanzishwa hii leo kwa msimu mpya wa ligi ya kandanda mjini Kyiv, baada ya michuano yote ya soka kusimamishwa toka Februari.