1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky asema Urusi imefyetua kombora la kuvuka mabara

21 Novemba 2024

Ukraine yaendelea kuchunguza kuthibitisha ikiwa kombora lililofyetuliwa na Urusi ni la masafa marefu la kuvuka mabara.

Shambulio la Urusi DNIPRO
Eneo lililoshambuliwa na Urusi-DniproPicha: Press Service of the State Emergency Service of Ukraine in Dnipr/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kiongozi wa Urusi, Vladmir Putin anaitumia Ukraine kama uwanja wa kufanyia majaribio silaha zake.

Tuhuma hizo za Zelensky amezitowa baada ya ripoti za jeshi la nchi yake kuonesha kwamba Urusi imeishambulia Ukraine kwa kutumia kombora la masafa marefu la kuvuka mabara.

Kombora la kuvuka mabara aina ya Yars la UrusiPicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Rais Zelensky amesema kwamba hivi sasa wataalamu wanafanya uchunguzi kupata uhakika juu ya kombora lililofyetuliwa leo asubuhi na Urusi, likiulenga mji wa Dnipro.

"Leo Urusi imefyetuwa kombora jingine. Dalili zote zinaashiria ni kombora la masafa marefu la kuvuka mabara. Uchunguzi wa wataalamu unaendelea. Ni wazi kwamba Putin anaitumia Ukraine kama uwanja wake wa kufanyia majaribio.''

Zelensky alikwenda mbali zaidi kwa kumuita Putin ni jirani mwendawazimu, aliyeamuwa kwa mara nyingine kujionesha ni mtu wa aina gani  na namna anavyochukia ustaarabu, uhuru, na maisha ya binadamu kwa ujumla wake na namna alivyo na khofu.

Ikiwa itathibishwa basi itakuwa ni mara ya kwanza Urusi kutumia silaha aiana hiyo katika vita hivyo vya kihistoria na bila shaka kuonesha vipi vita hivi vimeongezeka kwa kiasi kikubwa.Soma pia: Zelensky: Marekani ikipunguza ufadhili wake, tutashindwa vita dhidi ya Urusi

Makombora ya masafa marefu ya kisasa ya kuvuka mabara yameundwa kuwa na uwezo wa kubeba vichwa vya Nyuklia na kufika umbali wa wastani wa kilomita 5,500.

Silaha za Atomiki za Urusi zikioneshwa kwenye gwaride la kijeshiPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Taarifa za vyanzo na hata wataalamu waliozungumza na shirika la AFP zinaonesha waziwazi kwamba kombora lililofyetuliwa na Urusi halikubeba kicha cha Nyuklia, hivyo basi inaonesha nchi hiyo imefanya shambulio hilo kuleta taathira ya kisiasa.

Vituo vya matangazo vya Urusi vinavyotumia mtandao wa Telegram vimesema kwamba shambulio la Urusi liliyalenga miundo mbinu ya kijeshi ya Ukraine ikiwa ni pamoja na kampuni inayohusika na makombora na roketi ya Pivdenmash iliyo na makao makuu yake katika mji wa Dnipro.

Hata hivyo, mpaka sasa Urusi haijasema chochote kuhusu shambulio hilo.Soma pia: Urusi yasema utawala wa Biden umedhamiria kurefusha vita vya Ukraine

Mjini Brussels, Umoja wa Ulaya, umesema unafuatialia kujuwa ukweli juu ya shambulio hilo la Urusi lakini umeshapitisha kauli kwamba kilichofanywa na Urusi ni hatua ya wazi inayoonesha kutanuka kwa vita hivyo.

Msemaji wa masuala ya kigeni ndani ya umoja huo, Peter Stano amewaambia waandishi habari, shambulio hilo linaweza kubadili mkondo wa mambo katika vita hivi.

Makombora ya kuvuka mabara yakioneshwa Red Square-MoscowPicha: NATALIA KOLESNIKOVA/AFP

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ufaransa hakuweza kuthibitisha juu ya shambulio hilo la Urusi, ikiwa kombora la masafa marefu limetumika au la, lakini akaongeza kusema kwamba ikiwa itathibitika, kweli Urusi imefyetuwa kombora hilo itazidisha mgogoro huu na Ufaransa itachukuwa hatua zinazostahiki.