1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky adai wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini wako Kursk

5 Novemba 2024

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amedai kuwa wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini wamewasili katika mpaka wa nchi hiyo na Urusi kwenye eneo la Kursk, akihofia wanaweza kutumika na Urusi kuishambulia Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.Picha: Ukraine Presidency via Bestimage/IMAGO

Hadi sasa haijawa wazi iwapo wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaweza kuingizwa vitani katika maeneo ya Ukraine au katika maeneo ya Urusi yaliyotwaliwa na Ukraine, yanayojumuisha sehemu ya jimbo la Kursk. 

Marekani kwa upande wake inakadiria kuwa kuna  zaidi ya wanajeshi 12,000 wa Korea Kaskazini nchini Urusi huku 10,000 kati yao wakiwa Kursk.

Hata hivyo msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon, Brigedia Jeneali, Pat Ryder, amesema iwapo wanajeshi hao watatumika katika vita dhidi ya Ukraine watashambuliwa. 

Soma zaidi: Wanajeshi wa K. Kaskazini wajiandaai kuingia Ukraine

Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, alisema Pentagon ilikuwa inachunguza ripoti za madai ya oparesheni ya wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo hilo.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin.Picha: Press Service Of The President Of Ukraine/AP/picture alliance

Wanajeshi hao wa Pyongyang wanadaiwa kuwasili Urusi mwezi uliopita na kudaiwa pia kupewa mafunzo na vikosi vya Urusi na pia kupewa nguo za kijeshi za Urusi hii ikiwa ni kulingana na duru kutoka Marekani. 

Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini kupitia msemaji wake, Jeon Ha-kyou, ilisema ilikuwa inaamini wanajeshi hao wapo Urusi kuisadia nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya Ukraine. 

Ukraine yadunguwa droni 48 za Urusi

Kwengineko, jeshi la Ukraine limesema limedungua droni 48 kati ya 79 pamoja na makombora mawili yaliovurumishwa nchini humo na Urusi usiku wa kuamkia leo katika eneo la Kharkiv.

Gavana wake, Oleh Syniehubov, alisema shambulizi hilo la usiku liliwajeruhi watu wawili na kuharibu majengo matatu.

Wakaazi wa mji wa Krasylivka wakitengeza dirisha lao baada ya mashambulizi ya Urusi.Picha: Maksym Kishka/REUTERS

Shambulizi jengine katika jimbo la Sumy Kaskazini Mashariki mwa Ukraine liliharibu kituo cha mafuta. 

Soma zaidi: Zelensky asema wanajeshi 11,000 wa Pyongyang wako Kursk

Kando na hayo, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema japo Ukraine haina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia, inaweza kutengeneza "mabomu hatari" ambayo ni mchanganyiko wa vilipuzi vingi na nyenzo za mionzi.

Urusi imesema operesheni zake za kijeshi zimeizuwia Ukraine kuendelea na mpango wake wa kutaka kutengeneza silaha za nyuklia.

Ukraine ambayo iliachana na mpango wake huo kufuatia kuvunjika kwa muungano wa kisovieti ili kupata usalama wa mipaka yake imekanusha shutuma hizo za Urusi.

Ukraine imesema haijatoa kitisho chochote kwa Urusi kabla ya uvamizi kamili wa moscow nchini mwake mwaka 2022.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW