Zelensky adai wanajeshi wake wameikomboa Bakhmut
22 Septemba 2023Pamoja na kauli hiyo ya Zelensky, mpaka sasa hakuna ishara zinazoonesha kuwa majeshi ya Urusi yameondolewa katika mji huo. Wapiganaji wa Ukraine wamekuwa wakipambana kuvirejesha tena vijiji vya kaskazini na kusini vilivyo chini ya himaya ya Urusi.
Katika taarifa nyingine, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetoa taarifa kuwa kombora moja la Ukraine, limeishambulia kambi kuu ya wanamaji ya bandari ya Sevastopol katika rasi ya Crimea. Wizara hiyo imesema pia kuwa shambulio kubwa la kimtandao lilivuruga huduma za intaneti katika eneo hilo.
Soma zaidi: Makao makuu ya meli za Crimea yashambuliwa
Kwa upande wake, Idara ya mawasiliano ya Ukraine kupitia Jukwaa la Telegram imethibitisha kuhusika na shambulio lililoyalenga makao makuu ya jeshi la wanamaji la Urusi katika bandari hiyo.
Kando ya mwanajeshi mmoja aliyeripotiwa kutoweka baada ya shambuli la kombora, Gavana wa Sevastopol Mikhail Razvozhayev, amesema hakuna mtu yeyote aliyeumia katika makao makuu hayo ya jeshi la wanamaji yaliyokuwa yakiwaka moto.
Urusi: Tumezuia mashambulizi mengine ya makombora
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema pia kuwa, kando ya shambulio hilo, makombora matano yalidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi.
Tukisalia katika mzozo huo, meli ya mizigo ya Aroyat iling'oa nanga kutoka Ukraine, katika bandari ya Bahari Nyeusi ya Chornomorsk ikiwa imesheheni tani 17,600 za nafaka licha ya vizuizi vya Urusi. Naibu wa Waziri Mkuu wa Ukraine Olexandr Kubrakov amethibitisha hayo na ameandika kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa, meli hiyo iliyobeba bendera ya Palau, ni ya pili kuondoka na kuingia kwenye njia ya bahari ya muda iliyoundwa na Ukraine kama suluhisho la muda.
Kwa mujibu wa mamlaka ya kufuatilia safari za majini, Meli hiyo kwa sasa inapita kwenye Bahari Nyeusi na inajumuisha wahudumu kutoka mataifa ya Misri, Albania, Ubelgiji na Uturuki. Inatarajiwa kuwasili Alexandria, Misri Jumatano Ijayo.