1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky akosoa mazungumzo ya Scholz na Putin

Sylvia Mwehozi
16 Novemba 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameelezea kusikitishwa na mazungumzo ya nadra kwa njia ya simu kati ya Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Putin |Scholz
Rais wa Urusi Vladimir Putin -Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani Picha: Kay Nietfeld/Sputnik/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameelezea kusikitishwa na mazungumzo ya nadra kwa njia ya simu kati ya Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Rais wa Urusi Vladimir Putin, akisema mazungumzo kama hayo daima hayaelekei popote.

Katika ujumbe wake kwa njia ya vidio, Zelensky amesema kwa maoni yake, simu ya Scholz itafanya mambo kuwa magumu na kwamba mazungumzo kati ya Scholz na Putin huenda yakafungua njia ya mazungumzo zaidi, jambo ambalo Putin amekuwa akilitafuta kwa muda mrefu.

Kansela Scholz katika mazungumzo kwa njia ya simu na PutinPicha: Steffen Kugler/Bundesregierung/dpa/picture alliance

Zelensky hata hivyo alikiri kwamba alifahamishwa mapema kuhusu mazungumzo ya viongozi hao. Scholz alizungumza na Putin kwa muda wa saa moja siku ya  Ijumaa, hayo yakiwa ni mazungumzo ya kwanza kati ya viongozi hao wawili katika kipindi cha takriban miaka miwili.Scholz kukutana na Xi pembezoni mwa mkutano wa G20

Kulingana na Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit, Kansela Scholz aliitaka Urusi kuondoa wanajeshi wake kutoka Ukraine, kumaliza vita na kumtaka Putin kufanya mazungumzo na Ukraine kwa lengo la upatikanaji wa amani ya kudumu.

Scholz pia alisisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa Ukraine katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi ambao unaelekea kuwa wa muda mrefu na kwamba Putin asifikirie muda upo upande wake.

Wakati wa mazungumzo yake Kansela Scholz pia alimuonya Putin kwamba kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini kwa ajili ya mapigano nchini Ukraine au Urusi kutakuwa ni kuuzidisha vikali na kuupanua mzozo huo.Trump, Scholz wakubaliana kushirikiana katika kurejesha amani barani Ulaya

Muda mfupi kabla ya mazungumzo ya Ijumaa na Putin, hata hivyo, Scholz alisisitiza bungeni kwamba Ujerumani haitoipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ya Taurus, ambayo Ukraine imeomba mara kwa mara.

Kansela Schoz na Rais ZelenskyPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kulingana na Ikulu ya Kremlin, Putin alielezea nia yake kwa Scholz kufanya mazungumzo lakini chini ya mazingira yenye maslahi kwa Urusi.

Soma: Zelensky amshukuru Kansela Scholz katika mazungumzo yao

Alidai kwamba utatuzi wowote wa mzozo huo lazima uzingatie masilahi ya usalama ya Moscow na pia kuzingatia ukweli mpya kuhusu maeneo iliyoyatwaa ya mashariki na kusini mwa Ukraine.

Masharti yaliyotajwa na Putin pia yanaitaka Ukraine kuondokana na wazo la uanachama wa NATO, kulingana na Kremlin. Serikali ya Kiev hata hivyo imeyakataa masharti hayo.

Scholz anatafuta kufanya mkutano wa pili wa amani wa Ukraine, wakati huu akitaka kuwashirikisha maafisa wa Urusi, kufuatia mkutano wa kwanza uliofanyika nchini Uswisi wakati wa msimu wa joto uliopita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW