Zelensky afanya mazungumzo na Macron mjini Paris
1 Desemba 2025
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasili leo katika ikulu ya Elysee nchini Ufaransa kwa mazungumzo na Rais Emmanuel Macron kujaribu kupata uungaji mkono wa Ulaya kwa mpango wa amani wa kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine.
Ziara ya Zelensky nchini Ufaransa inakuja siku moja baada ya mazungumzo kati ya wajumbe wa Marekani na Ukraine huko Florida, na kabla ya mkutano kati ya mjumbe wa Marekani Steve Witkoff na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow.
Zelensky alifanya mazungumzo na Macron huku Ukraine ikitathmini maamuzi yake kuhusu mpango huo ulioungwa mkono na Rais wa Marekani Donald Trump lakini ambao nchi za Ulaya zinahofia kutumbukia katika matakwa ya Urusi.
Zelensky asema amani Ukraine lazima iwe ya kudumu
Rais Zelensky amesema mazungumzo yake ya saa kadhaa na Macron yaliangazia jinsi ya kumaliza vita, na kuongeza kuwa amani nchini Ukraine lazima iwe ya kudumu.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Zelensky amesema lazima vita iishe haraka iwezekanavyo na kwamba mengi sasa yanategemea ushiriki wa kila kiongozi.
Ameongeza kusema watazungumza na viongozi wengine hii leo.
Kwa upande wake, Macron ameandika ujumbe katika mtandao wa X, na kusema kuwa ''kazi ya amani inaendelea,".
Kallas asema mazungumzo ya Putin na Witkoff yanahatarisha shinikizo kwa Ukraine
Wakati wa mkutano na mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Kaja Kallas, amesema wiki hii inaweza kuwa muhimu kidiplomasia.
''Tulisikia jana kwamba mazungumzo nchini Marekani yalikuwa magumu lakini yenye tija. Bado hatujapata matokeo lakini nitazungumza na waziri wa ulinzi pamoja na wa mambo ya nje wa Ukraine hii leo.''
Hata hivyo Kallas ameonya kuwa mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff yanahatarisha kuiwekea Ukraine shinikizo la kuingia katika makubaliano.
Hapo jana, wajumbe wa Marekani na Ukraine walifanya mazungumzo ya saa kadhaa mjini Florida katika kile ambacho pande zote mbili kiliyataja kuwa ya tija huku Rais Donald Trump akiwa ndani ya ndege ya Air Force One akisema kuna nafasi nzuri ya uwezekano wa makubaliano.
Urusi yafanya mashambulizi mjini Dnipro
Watu wanne wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa katika shambulizi la kombora la Urusi kwenye mji wa Dnipro, mashariki ya kati mwa Ukraine.
Kupitia ujumbe kwenye mtandao wa Telegram, kaimu gavana wa mkoa jirani wa Dnipropetrovsk, Vladyslav Haivanenko, amesema watu 11 waliojeruhiwa kwenye shambulizi hilo wako mahututi .
Amesema shughuli ya utafutaji na uokoaji imekamilika.
Idara ya huduma za dharura ya Ukraine imesema vituo vya huduma za magari pamoja na biashara nyingine, jengo la ofisi na magari 49 pia yaliharibika wakati wa shambulizi hilo.
Picha zilizochapishwa kwenye mtandao wa Telegram zilionyesha maafisa wa zima moto wakijaribu kuzima moto katika eneo la mkasa na wale wa dharura wakiwahamisha watu kwenye machela.
Mji wa kiviwanda wa Dnipro na maeneo jirani yamekabiliwa na mashambhulizi ya mara kwa mara ya makombora na droni ambayo yamewauawa raia na kuharibu nyumba, viwanda na miundo mbinu.
Hakukuwa na taarifa ya haraka kutoka Urusi kuhusiana na shambulizi hilo.