1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky afanya ziara Izium

14 Septemba 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amefanya ziara ya ghafla katika eneo lilolokombolewa upya la Izium, kitovu muhimu cha vifaa kaskazini mashariki mwa mkoa wa Kharkiv.

Zelensky alishukuru jeshi lake kwa mafanikio katika kudhibiti tena eneo hilo kutoka kwa vikosi vya Urusi. soma Zelenskiy: Ukraine yakabiliwa na hasara chungu Severodonetsk, Kharkiv

Maelfu ya wanajeshi wa Urusi walikimbia mji wa Izium mwishoni mwa juma na kuacha nyuma kiasi kikubwa cha risasi na vifaa, katika kushindwa kwao vibaya zaidi tangu wafurushwe kutoka nje kidogo ya mji mkuu wa Ukraine Kyiv mwezi Machi.

soma Ukraine yawasukuma nyuma wanajeshi wa Urusi Kharkiv

Akizungumza kwenye sherehe ambapo bendera ya taifa ilipandishwa nje ya eneo la Izium Zelensky amesema ana imani kwamba wahusika wa uhalifu wa kivita watafikishwa mahakamani kufuatia uchunguzi wa waendesha mashtaka wa Ukraine pamoja na wa kimataifa.

Urusi yadai kufanya "mashambulio makubwa" Kharkiv

Picha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin Poo//AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Huku haya yakijiri msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Igor Konashenkov amedai kwamba wanajeshi wa nchi yake leo Jumatano wamekuwa wakifanya kile alichokitaja kama "mashambulio makubwa" katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Kharkiv.

Akizungumza mjini Moscow, Konashenkov alisema katika maeneo ya Dvorichna, Balakliya na Kupiansk, mashambulizi makubwa yalitekelezwa kwa kutumia zana za kijeshi na kwamba wanajeshi 150 wa Ukraine waliuawa na kujeruhiwa, na zaidi ya vitengo 10 vya zana za kijeshi viliharibiwa.Hata hivyo madai hayo hayakuweza kuthibitishwa.

"Maghala manne ya silaha za roketi na mizinga, pamoja na risasi katika maeneo ya Siversk na Raihorodok katika Jamuhuri ya Watu wa Donetsk, miji ya Kharkiv na Izyum katika mkoa wa Kharkiv iliharibiwa. Katika eneo la Krasnyy Liman la Jamuhuri ya Watu wa Donetsk, gari la mfumo wa roketi la Uragan liliharibiwa." alisema Konashenkov.

soma Shinikizo laongezeka dhidi ya India ilaani uvamizi wa Urusi

Katika mkutano na waandishi wa habari msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema kwamba matarajio yanayoendelea ya Ukraine ya kujiunga na Jumuiya ya kujihami ya  NATO  ulikuwa tishio kwa usalama wa Urusi na kuisababisha Urusi kufanya kile inachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.

Peskov ameongeza kusema kwamba Urusi iliitazama vibaya hati hiyo, na wazo la Ukraine kujiunga na NATO lilikuwa "tishio kuu kwa Urusi.

Kabla ya Urusi kutuma vikosi vyake vya kijeshi nchini Ukraine mnamo Februari, Moscow ilikuwa ikidai kuwa na dhamana ya kisheria kwa Ukraine kwamba kamwe haitakubaliwa katika muungano huo wa ulinzi wa bahari ya Atlantiki inayoongozwa na Marekani.

 

Reuters/

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW