1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Zelensky afanya ziara Ufilipino kusaka uungwaji mkono

3 Juni 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekutana na mwenzake wa Ufilipino Ferdinand Marcos katika ziara yake isiyokuwa ya kawaida barani Asia.

Ufilipino Manila |Volodoymyr Zelensky| Ferdinand Marcos Jr
Rais Volodoymyr Zelensky wa Ukraine (kushoto) akisalimiana na Rais Ferdinand Marcos Jr wa Ufilipino mjini Manila.Picha: Jam Sta Rosa/Pool/Getty Images

Ameitumia ziara hiyo kuwaomba viongozi wa bara hilo kuhudhuria mkutano wa kilele wa amani ulioandaliwa na Uswisi kujadili vita vya Ukraine na Urusi. Zelensky amedai Urusi na China zinajaribu kuudhoofisha mkutano huo.

Zelensky aliwasili mjini Manila siku ya Jumapili chini ya ulinzi mkali, baada ya kushiriki Jukwaa la Kimataifa la majadiliano ya usalama la Shangri -La mjini Singapore.

Alikaribishwa nchini Ufilipino kwa gwaride la heshima katika Ikulu ya rais kabla ya kukutana na rais Ferdinand Marcos Jr. Rais Marcos kupitia katibu wake wa mawasiliano Cheloy Garafil, aliahidi kwamba Ufilipino itahudhuria mkutano huo wa amani.

Haijawa wazi hadi sasa iwapo rais huyo atahudhuria mwenyewe katika mkutano huo au atamtuma mwakilishi. 

"Tumefarijika kwamba umepata nafasi ya kuitembelea ufilipino, Najua mzozo nchini mwako umechukua muda wako mwingi lakini nashukuru kukutana na wewe kujadili mambo yanayohusu nchi zetu na kupata njia ya kuyashughulikia, natamani tungekuwa tunakutana kwa mazingira bora zaidi lakini nafurahi kwamba umekuja kututembelea bwana rais."  alisema Rais Marcos wakati alipokutana na Zelesky.

Zelensky nae alimshukuru kwa kuridhia ufilipino kuhudhuria mkutano huo akisema hiyo ni shara njema kwamba yupo pamoja na watu wa Ukraine.

"Ahsante kwa mwaliko wako na tunashukuru kuwa katika nchi inayoiunga mkono Ukraine, uadilifu na uhuru wake. Asante sana kwa tamko lako kubwa na msimamo wako juu ya uvamizi huu wa Urusi katika maeneo yetu na asante kwa kutuunga mkono pamoja na mataifa ya Umoja wa Mataifa na maazimio yenu. Nafurai kusikia utashiriki mkutano wa amani hilo ndio jambo watu wetu wanalolitaka, kurejesha amani nyumbani." alisema Zelensky. 

Katika mkutano wa viongozi hao wawili rais Volodymyr Zelensky alidokeza kuwa Ukraine ina nia ya kufungua ubalozi wake mjini Manilla, hatua ambayo ilikaribishwa na Rais Marcos akisema itasaidia kutoa msaada zaidi kwa taifa hilo linalokumbwa na vita.

China yakanusha madai ya Zelensky kuudunisha mkutano wa Uswisi

Huku hayo yakiarifiwa China imekanusha madai yaliyotolewa na Zelensky kwamba inajaribu kuzuwia nchi nyengine kuhudhuria mkutano huo wa amani utakaojadili vita vya Ukraine utakaofanyika tarehe 15 na 16 mwezi Juni nchini Uswisi.

Msemaji wa Izara ya mambo ya nchi za nje ya China Mao Ning amesema msimamo wao uko wazi kabisa na hawana haja yoyote ya kuzinishinikiza nchi nyengine kutohudhuria.

Rais Volodoymyr Zelensky wa UkrainePicha: Nhac Nguyen/AFP/Getty Images

Wiki iliyopita China ilisema itakuwa vigumu kwa taifa hilokushiriki mkutano huo iwapi mshirika wake Urusi hatoshiriki. Ukraine inatarajia kupata uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa katika mkutano huo katika lengo lake la kupata msaada zaidi wa kusitisha uvamizi wa Urusi nchini mwake.

Kwengineko Ukraine imesema itawataka washirika wake kuwapa wanajeshi wake uhuru zaidi wa kushambulia maeneo ya kijeshi ndani ya Urusi baada ya Marekani kuondoa vikwazo vya matumizi ya baadhi ya silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema, bado hawajaruhusiwa kwa asilimia 100 kushambulia maana ruhusa iliyotolewa inakuja kwa masharti. Amesema wataendelea kushirikiana na washirika wao wa magharibi juu ya uwezekano wa kuongeza matumizi ya silaha hizo.

Wiki iliyopita, Washington iliipa ruhusa Ukraine kutumia silaha inazopewa na magharibi kushambulia baadhi ya maeneo za kijeshi ndani ya Urusi kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na mashambulizi ya Urusi katika jimbo la Kharkiv.

Wakati huo huo msemaji wa rais Zelensky amethibitisha kwamba kiongozi huyo atahudhuria mkutano wa kundi la nchi tajiri kiviwanda G7 utakaofanyika nchini Italia.

Msemaji huyo Sergiy Nikiforov amesema Zelensky atahudhuria mkutano huo utakaofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni yeye mwenyewe au kupitia mawasiliano ya vidio. Ajenda kuu ni njia za kutumia mali ya Urusi zilizozuiliwa  kuisaidia Ukraine inayohitaji msaada zaidi wa kijeshi kutoka kwa washirika wake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW