1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHungary

Zelensky atoa wito wa misaada zaidi ya kifedha

13 Desemba 2023

Rais wa Ukraine amezirai nchi washirika wa Umoja wa Ulaya na Marekani kuendelea kuiunga mkono Kiev katika wakati ambapo migawanyiko ya ndani ya Brussels na Washington inatishia kuzuia misaada zaidi nchini Ukraine.

Finnland | Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyj na Rais wa Finland Sauli Niinistö |
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mkutano wa pamoja na Rais wa Finland Sauli Niinistö na waandishi wa habari Picha: Heikki Saukkomaa/Lehtikuva/dpa/picture alliance

Wito kama huo pia ameutoa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, aliyewahimiza viongozi wa umoja huo kuipa misaada zaidi ya kifedha Ukraine na pia kuunga mkono azma yake ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya kuelekea mkutano wao wa kilele mjini Brussels kesho Alhamisi juu ya dhamira ya Ukraine kujiunga na umoja huo. 

Rais Zelensky ameyasema hayo kabla ya mkutano na viongozi wa Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden, ambapo anatarajiwa kuomba msaada zaidi wa kifedha kwa ajili ya utengezaji wa silaha.

Zelensky amewaambia waandishi wa habari baada ya kufanya mkutano na Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store kwamba, "hawezi kushinda bila ya msaada.”

Migawanyiko ndani ya EU na Washington yatishia kuzuia misaada kwa Ukraine

Wanajeshi wa Ukraine wakijiandaa kwa mashambulizi kuelekea eneo la BakhmutPicha: Diego H. Carcedo/Anadolu/picture alliance

Wito wake huo ameutoa katika wakati ambapo mizozo na migawanyiko ya ndani kwa ndani ya Marekani na Umoja wa Ulaya inatishia kuzuia misaada yenye thamani ya mabilioni ya dola kwenda Ukraine.

Oparesheni ya kijeshi ya Ukraine iliyofanyika mwezi Julai dhidi ya vikosi vya Urusi na ambayo haikutoa matokeo yaliyotarajiwa, ni moja ya sababu iliyomshurutisha Zelensky kuomba msaada zaidi.

Kiongozi huyo anatarajiwa kukutana baadaye leo na mfalme wa Norway Harald V kabla ya kufanya mkutano na viongozi watano wa mataifa ya Nordic.

Zelensky anawataka viongozi hao wa Nordic kuisaidia kifedha Ukraine kwa ajili ya kutengeneza silaha zinazofikia viwango vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Katika ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la The Financial Times la nchini Uingereza, viongozi watano wa ukanda wa Nordic wameeleza kuwa, "Ukraine haiwezi kujilinda yenyewe dhidi ya Urusi kwa maneno tu” na kwamba mafanikio ya vita hayawezi kupatikana bila ya silaha.

Soma pia: Zelensky ateta na Orban uanachama wa Ukraine Umoja wa Ulaya 

Zelensky, baada ya ziara ya Jumapili nchini Argentina kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais Javier Milei, alisafiri hadi Marekani katika jaribio lake la mwisho la kuomba msaada zaidi wa kijeshi kutoka Washington.

Hata hivyo, bunge la Marekani lililogawanyika bado halijaidhinisha msaada mpya wa dola bilioni 60 kwa Ukraine.

Tangu kuanza kwa vita kati ya Ukraine na Urusi mnamo Februari 2022, mataifa ya Nordic yamekuwa wafadhili wakubwa wa Kiev.

Wakati hayo yanaarifiwa, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameuhimiza umoja huo kuiunga mkono Ukraine kwa muda mrefu uwezekanavyo.

Kauli yake hiyo ameitoa kuelekea mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kesho Alhamisi.

"Lazima tuipe Ukraine kile inachohitaji ili kuwa na nguvu leo, na pia ili iwe na nguvu kesho kwenye meza ya mazungumzo wakati inapojadili juu ya utulivu na amani ya muda mrefu nchini Ukraine.”

Hungary yatishia kupinga uanachama wa Ukraine ndani ya EU

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: AFP

Hata hivyo, Hungary inaonekana kuwa na msimamo tofauti juu ya kuiongezea msaada zaidi Ukraine.

Hungary inapinga wazo la kuipatia Ukraine misaada zaidi ya kifedha na imekwenda mbali zaidi hata kutishia kupinga mipango ya kuiruhusu Ukraine kuwa mwanachama wa umoja huo.

Soma pia: Hungary na Slovakia zapinga msaada wa kifedha kutolewa Ukraine 

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza kwamba mkutano wa kesho wa kilele unafaa kufanya uamuzi wiki hii juu ya mazungumzo ya uanachama wa Ukraine pindi nchi hiyo itakapotimiza masharti iliyowekewa na umoja huo.

Ukraine ilipewa orodha ya masharti kadhaa ya kuyatekeleza kabla ya kuanza rasmi kwa mazungumzo kujiunga na Umoja wa Ulaya.