1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Zelensky ahutubia Baraza la Mawaziri la Uingereza

19 Julai 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepokea pongezi nyingi kutoka kwa mawaziri wa Uingereza, kama kiongozi wa kwanza wa kigeni kuhutubia baraza la mawaziri ana kwa ana tangu 1997.

Uingereza | Waziri Mkuu wa Uingereza Starmer und Waiziri wa Ulinzi Healey na rais Zelensky.
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, kushoto na Waziri wa Ulinzi John Healey, kulia, wakimpongeza Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy baada ya kuhutubia mkutano usio wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la Uingereza.Picha: Richard Pohle/AP Photo/picture alliance

Zelensky amewaeleza wanachama wa serikali mpya ya Labour hali ya nchini Ukraine baada ya kukaribishwa kwenye makazi na ofisi ya Waziri Mkuu Keir Starmer.

Alipomkaribisha Zelensky Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema:

"Tumetazama kumbukumbu, Hii ni mara ya kwanza katika karne hii kwa kiongozi wa kigeni kuhutubia ndani ya baraza la mawaziri la Uingereza, kwa hivyo unakaribishwa sana kwenye mkutano ambao kwetu sisi ni wa muhimu kabisa.

Zelensky ameishukuru Uingereza kwa msaada wake endelevu kwa nchi yake tangu vikosi vya Urusi vilipoivamia mnamo Februari 2022.

Haya yanajiri siku moja baada ya Zelensky kuwataka viongozi wa Ulaya kuendelea kuwa na umoja dhidi ya uvamizi wa Urusi, huku akitafuta usaidizi zaidi wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na silaha za anga zinazohitajika ili kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi.

"Ni ishara ambayo ni muhimu sana kwangu mimi na kwa Waukraine wote, kwamba tunaunga mkono na tuna imani na Uingereza na huu ni mkutano wa kwanza wa aina yake katika baraza la mawaziri la Uingereza."

"Nashukuru sana. Ni matumaini yangu kwamba mkutano huu na kazi ya serikali mpya ya Uingereza utafungua fursa zaidi kwa nchi zetu za Ukraine na Uingereza."

Msaada zaidi kwa Ukraine

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg akiwa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.Picha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, ikiwa ni pamoja na Uingereza, wamekuwa wakisitasita kuhusu Ukraine kutumia silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kama vile makombora kulenga ndani ya Urusi, kwa hofu ya kuzidisha mzozo huo.

Soma pia: Stoltenberg asema anataraji msaada wa kutosha kwa Ukraine kutoka NATO

Uingereza imeashiria kwamba vikosi vya Ukraine vinaweza kutumia makombora ya Storm Shadow inayowasambazia kwa mashambulizi ya kujihami. 

"Hotuba ya kihistoria" ya Zelensky, kama Starmer alivyoiita, imejiri wakati nchi 44 na Umoja wa Ulaya zikikubali kukabiliana na meli za Urusi zinazojificha ili kukwepa vikwazo vya kuzia biashara ya mafuta ya Urusi.

Kiongozi wa mwisho wa kigeni kulihutubia Baraza la Mawaziri la Uingereza alikuwa rais wa Marekani Bill Clinton mwaka 1997 baada ya aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair wa chama cha Labour kuingia madarakani ambaye pia alipata ushindi mkubwa dhidi ya chama cha wahafidhina cha Conservatives.