Zelensky aikosoa EU kwa kutokabiliana na Putin
23 Januari 2026
Zelensky ametoa matamshi hayo wakati wa hotuba yake katika kongamano la kiuchumi la Davos, baada ya kiongozi huyo kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump, mazungumzo ambayo anadai kuwa yamefikia makubaliano kuhusu jinsi hakikisho la usalama wa Marekanikwa Ukraine baada ya vita litakavyokuwa. Aidha, Zelensky hakufafanua kilichomo ndani ya makubaliano hayo, akisema tu kwamba yamekamilika na yako tayari kutiwa saini na viongozi hao na kupitishwa na mabunge ya Ukraine na Marekani.
"Tunataka kumaliza vita hivi. Na ndiyo maana nafikiri Rais Trump anaweza kufanya hivyo kwa sababu amezungumza na Putin. Si kila mtu anaweza kufanya mazungumzo lakini yeye amezungumza na Putin katika ngazi sawa. Nadhani Marekani ina nguvu zaidi kuliko Urusi na unaweza kuona matokeo ya vita hivi. Ndiyo maana nafikiri jeshi la Marekani ni imara zaidi kuliko jeshi la Urusi, kutokana na uzoefu wetu wa vita, wa kujilinda wenyewe."
Zelensky pia alitumia jukwaa hilo kuwakosoa vikali washirika wake wakuu wa Umoja wa Ulaya kwa kutochukua hatua. Bila kutaja nchi yoyote moja kwa moja, Zelensky amesema Umoja huo umeshindwa kukubaliana jinsi ya kutatua matatizo ya kimataifa, akitaja kwamba kumekuwa na mabishano yasiyoisha ndani ya muungano huo na mambo hayasemwi kwa uwazi, yanayozuia ulaya kuungana na kuzungumza kwa umoja ili kupata suluhusho la ukweli.
Wakati huo huo, Ikulu ya Urusi Kremlin imethibitisha kwamba maafisa wa Moscow, Ukraine na Marekani watafanya mazungumzo ya kiusalama leo Ijumaa huko Umoja wa Falme za Kiarabu, kufuatia mazungumzo marefu yaliyodumu usiku kucha mjini Moscow kati ya wajumbe wa Marekani wakiongozwa na mjumbe maalum Steve Witkoff na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Mazungumzo ya Moscow yalihusu mpango wa Marekani wa kumaliza vita vya Ukraine, ambapo Kremlin imesisitiza kwamba kutatua mizozo ya kimaeneo ni jambo muhimu kwa makubaliano yoyote ya amani. Mshauri wa kidiplomasia wa Kremlin Yuri Ushakov aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mazungumzo ya Witkoff na Putinyalikuwa "yenye tija katika kila nyanja."
"Kama Vladimir Putin alivyosisitiza, tuna nia ya dhati ya kutaka kutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia za kisiasa na kidiplomasia. Lakini hadi hilo litakapowezekana, Urusi itaendelea kufuatilia kwa uthabiti malengo yaliyoainishwa kwa ajili ya operesheni maalumu ya kijeshi uwanja wa vita, ambako vikosi vya Urusi vina udhibiti wa kimkakati."
Kwingineko, shambulio la droni limesababisha moto katika kituo cha kuhifadhia mafuta katika mji wa Penza, magharibi mwa Urusi, mapema Ijumaa bila kusababisha majeruhi yoyote. Maafisa hawakufafanua chanzo cha droni hizo, lakini wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kwamba ulinzi wake wa anga ulikuwa umezima angalau droni 12 za Ukraine usiku kucha, ikiwemo moja katika eneo la Penza. Ukraine, ambayo imekuwa ikilenga miundombinu ya nishati ya Urusi katika kipindi chote cha vita vilivyokaribia miaka minne katika jaribio la kudhoofisha nguvu za nchi hiyo, haikutoa maoni mara moja.