1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aishukuru Poland kwa kuisaidia Ukraine

Angela Mdungu
5 Aprili 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa ziarani Poland amesema anatumaini kuwa mipaka ya Poland na Ukraine itakuwa wazi. Amewashukuru watu wa Poland kwa msaada wa kihistoria

Polen, Warschau | Staatsbesuch von Wolodymyr Selenskyj mit Präsident Andrzej Duda
Picha: Aleksandra Szmigiel/REUTERS

Amesema hasa katika siku za mwanzo za vita ya Urusi dhidi ya Ukraine Poland ilifungua milango yake na hakukuwa na mipaka na kwamba huo ni mwanzo wa kutokuwepo kwa mipaka hata katika siku zijazo.

Rais Volodymyr Zelensky ametoa shukrani zake kwa Rais wa Poland Andrzej Duda na watu wa Poland kwa msaada aliouita wa kihistoria na kwamba nchi hiyo jirani inapaswa kuwa mshirika muhimu katika juhudi za kuijenga upya Ukraine mara tu uvamizi wa Urusi utakapokoma.

Katika ziara hiyo Rais wa Poland Andrzej Duda amemtunuku Zelensky tuzo ya heshima yajuu zaidi nchini humo ijulikanayo kama "White Eagle". Tuzo hiyo ni kutokana na juhudi za Zelensky za kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Soma zaidi:Poland yaongeza shinikizo la kutuma vifaru Ukraine

Poland imekuwa mmoja wa washirika madhubuti wa Ukraine ikijiweka mstari wa mbele kwa kuwashawishi washirika wanaosita sita kuipatia silaha nzito nchi hiyo iliyo kwenye mzozo na Urusi.

Msaada zaidi wa kivita kwa Ukraine

Rais wa Poland ametangaza pia leo kuwa nchi yake itakuwa tayari kutuma ndege zake za kivita aina ya MiG-29 nchini Ukraine hapo baadaye ikiwa bado kutakuwa na uhitaji. Tayari Poland ilishaahidi kupeleka ndege 14 za kivita nchini humo.

Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesem, yeyote anayeisaidia Urusi katika vita dhidi ya Ukraine atakuwa ameshirikiana na Urusi katika kukiuka sheria ya kimataifa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais Emmanuel Macron ameyasema hayo leo Jumatano akiwa katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini China. Ameelezea pia imani aliyonayo kwa China katika kusaidia kutatua mvutano wa Urusi na Ukraine.

Wakati huohuo waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema leo kuwa atazungumza na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu yanayoendelea kwenye vita ya Ukraine atakapoitembelea Uturuki wiki hii. Cavusoglu amesema, Uturuki inafanya kazi na Umoja wa Mataifa kutatua masuala yanayohusiana na usafirishaji wa nafaka na mbolea kupitia bahari nyeusi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW