Zelensky akutana na Macron kusaka uungwaji mkono kwa Ukraine
1 Desemba 2025
Ziara ya Zelensky ni juhudi za hivi karibuni zaidi kusaka uungwaji mkono wa Ulaya, mnamo wakati rais wa Marekani Donald Trump akielezea matumaini ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine.
Wajumbe wa Marekani na Ukraine walifanya mazungumzo jana Jumapili ambayo pande zote mbili zilitaja kuwa 'yenye tija' huko Florida kuhusu mpango ambao Washington inataka kuwa msingi wa makubaliano ya amani kati ya Urusi na Ukraine.
Juhudi hizo za kidiplomasia zinajiri baada ya takriban miaka minne ya mgogoro huo na mnamo wakati Ukraine ikikabiliwa na sakata la ufisadi wa ndani, hali ambayo imemlazimisha Zelensky kumfuta kazi msaidizi wake wa karibu na mpatanishi mkuu katika juhudi za kutaka kumaliza vita.
Zelensky amekuwa akifanya ziara ya mara kwa mara nchini Ufaransa kuzungumza na Emmanuel Macron tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya nchi yake mnamo Februari 2022.