1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky ana mashaka ahadi ya Urusi kupunguza mashambulizi

30 Machi 2022

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema kwamba mazungumzo ya amani kati ya wapatanishi wa nchi yake na Urusi yameonesha mwelekeo mzuri, ingawa ameonya kuwa Urusi haiwezi kuaminiwa.

Ukraine-Krieg | Trümmer eines Lagers mit mehr als 50.000 Tonnen Tiefkühlkost in der Stadt Browary
Picha: Genya Savilov/AFP/Getty Images

Baada ya mazungumzo hayo ya Jumanne yaliyofanyika Istanbul, Uturuki, Urusi ilitangaza kuwa itapunguza kwa kiasi kikubwa operesheni za kijeshi karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kiev na mji wa kaskazini wa Chernihiv. Akizungumza Jumanne usiku kwa njia ya video, Zelensky amesema vitendo vya ujasiri na madhubuti vya wanajeshi wa Ukraine ake karibu na Kiev na Chernihiv.

Kwa mujibu wa Zelensky, Ukraine itaendeleza mchakato wa mazungumzo ya amani kwa kiwango wanachokitegemea wao, lakini amesisitiza kuhusu kutokuaminika kwa matamshi ya wawakilishi wa nchi ambayo bado inaendelea kufanya mashambulizi na kuwaangamiza. Amesema wawakilishi wa Ukraine hawatofikia makubaliano ya kuuza uhuru na uadilifu wa eneo lao.

Aidha, kiongozi huyo wa Ukraine amesema hapawezi kuwepo na mazungumzo ya kuiondolea Urusi vikwazo ilivyowekewa kutokana na uvamizi wake Ukraine, hadi hapo vita vitakapomalizika. Zelensky amesema suala la vikwazo haliwezi kuibuliwa hadi pale watakapopata kile kilicho chao na hadi vita viishe.

Ujumbe wa Urusi na Ukraine katika mazungumzo ya amani Istanbul, UturukiPicha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Urusi kwa upande wake imesema mazungumzo hayo yalikuwa ya ''kujenga.'' Mazungumzo ya jana yalidumu kwa muda wa saa nne huku kukiwa na mapumziko ya hapa na pale. Hayo yalikuwa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana baina ya pande hizo mbili katika wiki kadhaa. Mazungumzo kati ya ujumbe wa Urusi na Ukraine yanatarajiwa kuendelea Jumatano.

Marekani imesema baadhi ya majeshi ya Urusi yanaondoka Kiev

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, John Kirby, amesema anaamini kuwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi tayari wameanza kuondoka Ukraine. Akizungumza na waandishi habari, Kirby amesema kutokana na tangazo la Urusi la kuwaondoa wanajeshi wake Kiev na Chernihiv, wamegundua idadi ndogo ya wanajeshi imeanza kuondoka taratibu kutoka Kiev.

Soma zaidi: Urusi yazidisha mashambulizi Kiev

Hata hivyo, amesema wanaamini huko ni kujipanga upya, na sio kuondoka kabisa na kwamba wote wanapaswa kuwa tayari kuangalia mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo mengine ya Ukraine. Kwa mujibu wa Kirby, haimaanishi kuwa kitisho kwa Kiev kimemalizika. Amesema mashambulizi ya anga ya Urusi bado yanaendelea.

Awali, Rais wa Marekani, Joe Biden alisema hana uhakika kwamba ahadi ya Urusi kupunguza operesheni za kijeshi Kiev kutasababisha mabadiliko makubwa katika mzozo huo. Akizungumza na waandishi habari baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia, Biden amesemea kwa pamoja wameelezea mashaka yao kutokana na tangazo hilo la Urusi na wanasubiri kuona kitakachotokea.

Vita vya Ukraine vyavuruga mipango ya chakula ya WFP

Ama kwa upande mwingine Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP David Beasley ameonya kuwa vita vya Ukraine vinatishia kuzivuruga juhudi za shirika hilo kuwalisha takribani watu milioni 125 duniani kote kwa sababu Ukraine imetoka kuwa mlimaji wa nafaka ulimwenguni na kuwa kwenye foleni ya watu wanaosubiri msaada wa chakula.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP David BeasleyPicha: Domenico Stinellis/AP Photo/picture alliance

Beasley ameliambia Jumanne Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba asilimia 50 ya nafaka inayonunuliwa na WFP inatoka Ukraine, hivyo ni wazi mipango ya shirika hilo inavurugika.

Amesema vita hivyo, haviiangamizi tu Ukraine na eneo hilo, bali pia vina athari kwa muktadha wa kimataifa ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Beasley amesema wakulima wana hali duni, hivyo nao wanahitaji msaada wa chakula. Amesema mzozo huo umechangiwa na ukosefu wa bidhaa za mbolea zinazotoka Belarus na Urusi.

Kabla ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari 24, WFP tayari ilikuwa inakabiliwa na bei ya juu ya mafuta na vyakula pamoja na gharama za usafirishaji ambayo ilisababisha shirika hilo kupunguza mgao wa chakula kwa mamilioni ya watu katika maeneo yenye mizozo ikiwemo Yemen na maeneo kadhaa ya Afrika. Beasley ameonya kuwa iwapo vita vya Ukraine havitamalizika, dunia itashuhudia WFP ikichukua chakula kutoka kwa watoto wanaohitaji chakula na kuwapa watoto wanaokufa kwa njaa zaidi.

(AFP, DPA, AP, Reuters)