1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aomba silaha zaidi kukabiliana na uvamizi wa Urusi

10 Oktoba 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito kwa washirika wake kuchukua hatua madhubuti baada ya Urusi kushambulia tena miundombinu ya nishati ya Ukraine. Mtu mmoja ameuwawa na angalau watu 12 wamejeruhiwa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Ukraine yatoa wito kwa washirika wake kuchukua hatua madhubuti baada ya Urusi kushambulia tena miundombinu yake ya nishati. Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Rais Volodymyr Zelenskyy amesema: "Kinachohitajika ni hatua thabiti kutoka Marekani, Ulaya na nchi wanachama wa kundi la G7 katika kufikisha mifumo ya ulinzi wa anga na kuiwekea Urusi vikwazo vikali zaidi.

Zelensky amesemaUrusi imerusha zaidi ya droni 450 na makombora zaidi ya 30 katika mashambulio ya usiku kucha. Jeshi la anga la Ukraine limesema mji mkuu Kyiv umeshambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Urusi, na limewahimiza wakazi wa mji huo kubaki kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya usalama.

Meya wa jiji la Kiyv Vitali Klitschko amesema sehemu ya upande wa kushoto wa Mto Dnipro katika mji huo hazina hudum za umeme na maji ambazo zimekatizwa kutokana na mashambulizi hayo. Watu 12 walijeruhiwa, wanane kati yao wakipelekwa hospitalini, huku majengo kadhaa ya makazi yakiteketea kwa moto au kuharibiwa.

Gavana wa mkoa wa Zaporizhzhya, Ivan Fedorov, amethibitisha mauaji ya mtoto wa miaka saba katika mashambulizi yaliyodumu zaidi ya saa sitaPicha: Bart Maat/ANP/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Zaporizhzhya, Ivan Fedorov, pia alisema kupitia Telegram kwamba katika eneo hilo, mtoto wa miaka saba aliuwawa na wengine wawili kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyodumu zaidi ya saa sita, ambapo nyumba binafsi na miundombinu ya nishati zililengwa. Katika mkoa wa Dnipropetrovsk, Urusi pia ilishambulia miundombinu ya umeme, na kumjeruhi mwanaume mmoja huku ikisababisha milipuko ya moto kadhaa, kulingana na gavana wa eneo hilo, Serhiy Lysak.

Waziri wa Nishati wa Ukraine, Svitlana Grynchuk, kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema kwamba vikosi vya Urusi vinafanya "shambulio kubwa” dhidi ya vituo vya nishati vya nchi hiyo, akitoa hakikisho kuwa "wafanyakazi wa sekta ya nishati wanachukua hatua zote muhimu kupunguza athari hasi.” Meya wa Sloviansk Vadym Lyakh, ametoa wito wa tahadhari kwa umma wakati taifa hilo linapoendelea kuikabili hali.

Vikosi vya Urusi vimeendelea kulenga miundombinu muhimu ya Ukraine

"Ninawashauri wakazi hasa wazee na familia zilizo na watoto — ni wakati wa kuondoka. Angalau kwa kipindi cha msimu unaohitaji joto la nyumba, kwa sababu tunaona adui analenga mfumo wa nishati, hususan mitambo ya majokofu na mabwawa ya mvuke. Hili linaweka hatari kubwa kwamba msimu wa joto la nyumba utakuwa mgumu sana. Kaeni imara. Tuko pamoja katika hili. Kadri msimu mwingine wa baridi unavyokaribia, vikosi vya Urusi vimeendelea kulenga miundombinu muhimu ya Ukraine huku uvamizi ukiendelea. Jilindeni.”

Hata hivyo, Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais Zelenskyy, Andriy Yermak, alisema Alhamisi kwamba watoto na vijana 23 wa Kiukraine wameondolewa kutoka maeneo yanayokaliwa na Urusi hadi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Kyiv.

 

Kupitia ujumbe kwenye programu ya Telegram, Yermak alisema uokoaji huo ulifanywa chini ya mpango wa rais uitwao "Bring Kids Back UA”, unaolenga kuwarejesha watoto waliotekwa au kufungwa katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi hadi sehemu salama.

Ukraine inasema Urusi imewapora au kuwahamisha kwa nguvu zaidi ya watoto 19,500 kwenda Urusi na Belarus,jambo linalokiuka Mkataba wa Geneva, ingawa Urusi inakanusha madai hayo ikidai kuwa imewachukua watoto hao kuwakinga dhidi ya hatari za vita.

Kadri vita vinavyoendelea, Kamanda wa Jeshi la Ukraine, Oleksandr Syrskyi, alisema Ukraine ilishambulia malengo ndani ya Urusi mara 70 mwezi uliopita, na kuharibu uzalishaji wa mafuta, vilainishi, vilipuzi, na vipengele vingine vya sekta ya kijeshi ya Urusi, hivyo kupunguza uwezo wa usafishaji mafuta nchini humo kwa asilimia 21.

Ukraine imekuwa ikijitetea kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu dhidi ya uvamizi kamili wa Urusi.