1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelensky atishia kuishambulia zaidi Urusi kwa droni

28 Oktoba 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameonya jana kwamba Kiev inapanga kupanua mashambulizi yake ya Droni na makombora katika mikoa zaidi ya Urusi.

Ukraine Donetsk 2025 | Makamanda wa vikosi vya uvamizi wakiwasilisha beret mpya
Makamanda wa vikosi vya uvamizi wakiwasilisha beret mpyaPicha: Office of the president of Ukraine

Rais wa UkraineVolodymyr Zelensky ameonya jana kwamba Kiev inapanga kupanua mashambulizi yake ya Droni na makombora katika mikoa zaidi ya Urusi. Katika ujumbe wake wa vidio kwa taifa, Zelensky alisema kwamba "uwezo wa mashambulizi ya masafa marefu ni sehemu ya uhuru wa nchi hiyo na itakuwa ni kiungo muhimu sana katika kuamua amani ya nchi".

Zelenksy ameongeza kuwa viongozi wa kijeshi walikuwa wamejadili maeneo ya kufanya mashambulizi hadi mwisho wa mwaka ikiwa ni pamoja na "upanuzi wa kijiografia" wa mashambulizi.

Hata hivyo, siku moja kabla, kiongozi huyo wa Ukraine alikiri kwamba nchi hiyo inakabiliwa "na tatizo la kiufundi" katika utengenezaji wa makombora ya masafa marefu yaliyoyopangwa kwa muda mrefu yanayofahamika kama Flamingo.

Mkoa wa Urusi wa Belgorod baada ya kushambuliwa na UkrainePicha: Governor of Belgorod Region Vyacheslav Gladkov via Telegram/via REUTERS

Mamlaka za Urusi zimetangaza hali ya dharura hapo jana baada ya bwawa moja katika mkoa wake wa Belgorod karibu na mpaka na Ukraine kuharibiwa na mashambulizi ya droni ya Kiev.

Mamlaka zinazosimamia maji zimelieleza shirika la habari la TASS kwamba kiwango cha maji katika bwawa hilo kimepungua kwa mita moja huku Gavana wa mkoa huo akiwataka wakaazi wanaoishi chini ya bwawa hilo kuchukua tahadhari.

Amesema maji kutoka katika bwawa hilo yamefurika katika maeneo ya Urusi karibu na kijiji cha Grafovka. Kutoka hapo maji hutiririka kuingia katika maeneo ya Ukraine ambako vikosi vya Urusi vinashikilia daraja dogo karibu na Vovchansk tangu mwaka 2024.

Wakati huo huo, ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana imesema kwamba Urusi imetenda uhalifu dhidi ya ubinadaamukwa kuwalazimisha watu kukimbia eneo la Ukraine inalolidhibiti kupitia mashambulizi ya mara kwa mara ya droni yanayolenga raia.

Tume hiyo huru ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ukraine pia imebaini kwamba Urusi ilitenda uhalifu wa kivita katika kuwahamisha na kuwasafirisha raia kutoka maeneo yanayokaliwa ya mkoa wa Ukraine wa  Zaporizhzhia.

Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Alexander Kazakov/Sputnik/REUTERS

Ripoti hiyo iliongeza kwamba "mamlaka za Urusi zimeratibu hatua za kimfumo za kuwaondoa raia wa Ukraine kutoka katika makaazi yao kwa kufanya mashambulizi ya droni, pamoja na kuwafukuza na kuwahamisha".

Tume hiyo ilianzishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa muda mfupi baada ya Moscow kuanza uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022.

Na kampuni kubwa ya mafuta ya Urusi ya Lukoil imesema jumatatu jioni kwamba itauza mali zake za nje ya nchi, baada ya kulengwa na vikwazo vya Marekanikutokana na vita vyake nchini Ukraine.

Wiki iliyopita Rais Donald Trump alitangaza vikwazo vya kwanza dhidi ya Urusi, akiyalenga makampuni mawili ya mafuta ya Lukoil na Rosneft baada ya kusema kwamba amekasirishwa na hatua ya Moscow ya kutokomesha mashambulizi yake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW