1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky apendekeza makubaliano ya fidia kutoka Urusi

21 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy Ijumaa alipendekeza makubaliano rasmi na washirika wa nchi hiyo ili kupata fidia ya Urusi kwa uharibifu uliofanywa na vikosi vyake wakati wa vita nchini humo.

Ukraine Kiew Präsident Volodymyr Zelensky Ansprache
Picha: REUTERS

Zelenskiy, ambaye anasema Urusi inajaribu kuharibu miundombinu ya Ukraine kwa kadri inavyoweza, ameongeza kuwa mpango kama huo utaonyesha mataifa yanayopanga vitendo vya uchokozi kwamba yatalazimika kulipia matendo yao. Katika hotuba yake kupitia njia ya video, Zelenskiy amesema kuwa wanakaribisha  mataifa yote washirika kutia saini makubaliano ya kimataifa na kuunda utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtu aliyeathirika kutokana na vitendo vya Urusi anaweza kupokea fidia kwa hasara aliyopata.

Zelenskiy amesema chini ya makubaliano kama hayo, pesa na mali ya Urusi katika mataifa yaliotia saini makubaliano hayo zitazuiwa na kuelekezwa katika hazina maalumu ya fidia. Mwezi uliopita, Canada ilisema kuwa itabadilisha sheria zake za vikwazo kuwezesha mali ya nje iliyozuiwa kutumiwa kama fidia kwa waathiriwa ama kusaidia taifa la nje kujijenga upya baada ya vita.

Kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini MariupolPicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Urusi yadai kuchukuwa udhibiti Mariupol

Huku hayo yakijiri, Urusi Ijumaa imedai kuchukuwa udhibiti wa mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine katika kile kitakachokuwa ushindi mkubwa zaidi katika vita vyake na Ukraine baada ya takriban miezi mitatu ya mapigano yaliosababisha uharibifu mkubwa katika mji huo na vifo vya takriban raia elfu 20. Waziri wa ulinzi wa Urusi  Sergei Shoigu aliripoti kwa rais Vladimir Putin ''ukombozi kamili'' wa kiwanda cha chuma cha  Azovstal huko Mariupol hii ikiwa ngome ya mwisho ya Ukraine. Haya ni kwa mujibu wa msemaji wizara ya ulinzi ya Ukraine Igor Konashenkov.

Hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka Ukraine.

Shirika la habari la serikali ya Urusi RIA Novosti limeinukuu wizara hiyo ya ulinzi ikisema takriban wapiganaji 2,439 wa Ukraine waliokuwa wamejificha katika kiwanda hicho cha chuma walijisalimisha tangu Jumatatu ikiwa ni pamoja na wengine zaidi ya 500 waliojisalimisha Ijumaa. Wakati wa kujisalimisha, wanajeshi hao walichukuliwa kama wafungwa na vikosi vya Urusi na baadhi yao wanasemekana kulazwa hospitalini.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW