1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky hatokubali makubaliano ya amani bila Ukraine

13 Februari 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema leo Alhamisi kwamba hatokubali makubaliano yoyote kuhusu Ukraine ambayo hayataijumuisha nchi hiyo katika ngazi ya mazungumzo.

Belgien Brüssel 2024 | Selenskyj gibt Pressekonferenz nach EU-Gipfeltreffen
Picha: John Thys/AFP

Katika kauli yake ya kwanza kwa waandishi habari tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipofanya mazungumzo ya saa nzima kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin hapo jana kabla ya kumpigia pia Zelensky, kiongozi huyo wa Ukraine amesema kitu muhimu kilikuwa ni kutoyaendesha mambo chini ya mpango wa Putin. Zelensky amesema Ukraine kama nchi huru haiwezi kukubali makubaliano ya aina yoyote au mazungumzo yoyote yatakayofanywa kuijadili nchi yake bila kuihusisha moja kwa moja.

Kiev na washirika wake wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kwamba wajumuishwe katika mazungumzo ya amani yatakayoijadili Ukraine. Baada ya mazungumzo na Putin, Rais Trump alisema Ukraine haiwezi kudhibiti tena maeneo yake yote na wala kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami NATO.

Ukraine yasisitiza kukubaliwa ombi lake la kutaka kuwa mwanachama wa NATO

Tamko la Trump limeishitua Ulaya inayotaka kuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo ya kusitisha vita vya Urusi na Ukraine, kwa sababu makubaliano yoyote ya kusitisha vita baina ya nchi hizo mbili hasimu vilivyoanza miaka mitatu iliyopita huenda yakawa na athari kwa usalama wa Ulaya.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas amesema sasa ni wazi kwamba makubaliano yote yatakayofanywa bila umoja huo na Ukraine yenyewe kuhusishwa yatafeli. Akizungumza mjini Brussels kunakofanyika mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO amehoji ni kwa nini Urusi inapewa kile inachokitaka hata kabla ya majadiliano kuanza?

Marekani: Ukraine kujiunga na NATO haitokuwa sehemu ya mazungumzo ya kutafuta amani

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete HegsethPicha: AdMedia/Newscom/IMAGO

Awali Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth alisema haiingii akilini kwa Urusi kurejea katika maeneo ya mipaka yake kabla ya mwaka 2014, na kwamba suala la taifa hilo kujiunga na NATO halitokuwa sehemu ya mazungumzo ya kutafuta amani. Urusi ililinyakua eneo la Crimea la Ukraine mwaka 2014. Kutokana na hayo Kaja Kallasamesema Ulaya itaendelea kuiunga mkono Ukraine iwapo haitokubali makubaliano ya aina yoyote kutoka kwa Trump na Putin.

Umoja wa Ulaya waidhinisha kurefushwa muda wa vikwazo dhidi ya Urusi

Ujerumani nayo imesema Marekani isingekuwa na makubaliano na Urusi kabla ya mazungumzo rasmi kufanyika. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema mpango wa kumaliza vita vya Ukraine haupaswi kulazimishwa kwa Kiev akionya kuwa ni lazima kila mtu ajue kuwa haiwezekani kuwa na amani ya kulazimishwa.

Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, amesema ni muhimu kwa Ukraine kuwa katika nafasi ya juu ya majadiliano iwe ni katika kusitisha vita au kuendelea na mapambano. Urusi kupitia naibu Mwenyekiti wa Baraza lililo na nguvu la Usalama nchini humo Dmitry Medvedev, imesema maongezi kati ya Trump na Putin yanaonyesha kuwa nia ya Ulaya ya kutaka kuishinda Urusi haitawahi kufanikiwa.

SIku 1,000 za vita vya Ukraine

01:44

This browser does not support the video element.

ap/ afp/ reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW