Zelensky asema makubaliano ya amani yamefikia asilimia 90
1 Januari 2026
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema makubaliano ya amani kati ya nchi yake na Urusi yamefikia asilimia 90 lakini amekumbusha kuwa masuala muhimu zaidi bado hayajatatuliwa na makubaliano yoyote hayapaswi kuipa ushindi Urusi.
Katika taarifa aliyoichapisha katika mtandao wa kijamii wa Telegram kuwatakia heri ya mwaka mpya raia wa nchi yake, Zelensky ameweka wazi kwamba nchi yake inataka kufikia ukomo wa vita hivyo lakini si kwa gharama yoyote na ni muhimu kwa nchi yake kupewa dhamana ya usalama na kuizuia Urusi kuivamia tena.
Katika hatua hatua nyingine, mjumbe maalum wa Marekani anayeshughulika na mzozo huo, Steve Witkoff hapo jana amejadili hatua zinazofuata za namna ya kuvimaliza vita hivyo na washauri wa serikali za Ulaya.
Mzozo wa Urusi na Ukraine una karibu miaka minne sasa na licha ya jitihada mbalimbali kufanyika lakini bado nchi hizo zimeendelea kushambiliana kwa makombora.