1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky asema serikali yake inahitaji "nguvu mpya"

4 Septemba 2024

Rais Volodymyr Zelensky amesema serikali yake inahitaji nguvu mpya na hatua ya kulifanyia mageuzi baraza lake la mawaziri katika wakati muhimu wa vita dhidi ya Urusi.

Zelensky-Ukraine
Rais wa Volodymr Zelensky asema serikali yake inahitaji "nguvu mpya" Picha: Juan Carlos Rojas/picture alliance

Mpango wa Rais Zelensky kutaka kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri, umesababisha mawaziri kadhaa kujiuzulu. Kufikia sasa jumla ya mawaziri sita, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba, naibu waziri anayeshughulikia masuala ya ushirikiano wa Ulaya, waziri wa viwanda anayesimamia uzalishaji wa silaha Ukraine na wengine wawili, waliwasilisha maombi ya kujiuzulu na bunge hii leo limeridhia kujiuzulu kwao.

Soma pia: Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba awasilisha barua ya kujiuzulu

Hata hivyo, bunge la Ukraine limesema kwamba litazingatia ombi la Kuleba kujiuzulu kesho Alhamisi.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Ireland Simon Harris mjini Kyiv, Zelensky amewashukuru waliojiuzulu kwa kazi yao.

"Ninawashukuru sana mawaziri na timu nzima ya Baraza la Mawaziri ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa ajili ya Waukraine, kwa miaka minne na nusu, na baadhi yao wamekuwa mawaziri wetu kwa miaka mitano, na sasa tunahitaji nguvu mpya. Na hatua hizi zinahusiana na kuimarisha maeneo yetu pamoja na  diplomasia na siasa za kimataifa."

Jukumu jipya kwa Kuleba?

Uvumi unaenea kwamba huenda Kuleba atapewa jukumu jipya katika serikali ya Ukraine.Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Kwa mujibu wa chanzo karibu na ofisi ya rais, Zelensky na Kuleba "watajadili na kuamua" wadhifa wake wa baadaye, wakati uvumi ukienea kwamba Kuleba anaweza kupewa jukumu la kuongoza ombi la Ukraine la kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Kremlin imesema kwamba mabadiliko ya serikali nchini Ukraine hayataathiri mchakato wa mazungumzo ya amani kwa njia yoyote, ingawa mazungumzo yanaonekana kufifia.

Soma pia: Zelensky: Hakuna maana yoyote kufanya mazungumzo na Putin

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema amesikitishwa na taarifa ya kujiuzulu kwa mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba na kumtakia heri.

Mashambulizi yazidi kupamba moto

Haya yanajiri wakati vikosi vya Urusi vinazidi kusonga mbele mashariki mwa Ukraine wakati wanajeshi wa Ukraine wakifanya uvamizi katika eneo la Kursk la Urusi. 

Mashambulizi yaendelea katika mji wa Lviv na majengo ya kihistoria kuharibiwa.Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Urusi imefanya mashambulizi katika mji wa Lviv, magharibi mwa Ukraine na kusababisha vifo vya watu saba na wengine 40 kujeruhiwa na kuharibu majengo kadhaa ya kihistoria.

Kupitia mtandao wa Telegram, waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Igor Klymenko, amesema operesheni ya uokoaji na kutafuta manusura inaendelea.