1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

Zelensky: Niko tayari kukutana na Putin kwa mazungumzo

12 Mei 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini Uturuki mnamo siku ya Alhamisi kwa mazungumzo ya moja kwa moja ya kumaliza vita kati ya nchi hizo mbili.

Ukraine | Europäische Führungskräfte in Kiew | Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: LUDOVIC MARIN/POOL/AFP

Kauli yake hiyo aliyoiandika kupitia mtandao wa kijamii wa X, imekuja muda mfupi baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuihimiza Ukraine kukubali pendekezo la Putin la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja nchini Uturuki. 

Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa wanasubiri usitishaji kamili na wa kudumu wa mapigano kuanzia leo Jumatatu, ili kutoa msingi unaohitajika kwa diplomasia.

Soma pia: Ukraine: Tupo tayari kusitisha mapigano kwa siku 30

Kiongozi huyo wa Ukraine ameongeza kuwa, hakuna maana ya kuendeleza mauaji.

"Nitakuwepo nchini Uturuki Alhamisi hii, tarehe 15 Mei, na nitamsubiri Putin nchini Uturuki. Binafsi. Naamini kuwa safari hii Putin hatatafuta visingizio vya kutofanya jambo fulani. Tuko tayari kuzungumza ili kumaliza vita. Alhamisi, Uturuki. Rais Trump ameonyesha uungwaji mkono wake. Viongozi wote wanaunga mkono hili."

Hata hivyo hakukuwa na majibu yoyote kutoka Ikulu ya Kremlin kuhusu utayari wa Zelensky kuzungumza na Putin.

Washirika wa Kyiv wasisitiza kuwepo kwa usitishaji mapigano

Zelensky na viongozi wa Ulaya walichukua msimamo mwishoni mwa wiki kwamba hakutafanyika mazungumzo yoyote hadi Putin atakapokubali mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30 bila masharti kuanzia leo Jumatatu.

Urusi na Ukraine hazifanya mazungumzo ya ana kwa ana tangu Machi mwaka 2022, muda mfupi baada ya Kremlin kufanya uvamizi kamili mnamo mwezi Februari mwaka huo.

Mapema jana, Putin alipendekeza kurejea tena kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliyofanyika mjini Istanbul mnamo Machi, mwaka 2022. Hata hivyo, hakutoa jibu kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30 lililotolewa na washirika wa Ukraine.

Soma pia: Urusi na Ukraine zashambuliana licha ya juhudi za upatanishi

Rais wa Marekani Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth kwamba, "Rais Putin wa Urusi hataki kuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano na Ukraine, bali anataka kufanya mkutano siku ya Alhamisi nchini Uturuki, kujadili uwezekano wa kumaliza umwagikaji damu.”

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Kiongozi huyo wa Marekani ameongeza kuwa, "Ukraine inapaswa kukubaliana na hili, mara moja. Angalau wataweza kubaini iwapo makubaliano hayo yanawezekana au la, na iwapo itakuwa hivyo, viongozi wa Ulaya na Marekani, watajua hali halisi na kuchukua hatua stahiki.”

Ukraine na washirika wake wa Magharibi wameeleza kuwa, mpango wa usitishaji mapigano usio na masharti ndio njia pekee ya kuendelea na suluhisho la kidiplomasia katika kuutafutia ufumbuzi mzozo huo ulioingia mwaka wake wa tatu – vita vibaya zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Mashambulizi ya Urusi yamesababisha vifo vya mamia ya watu, uharibifu wa miji ya Ukraine na kuporomoka kwa mahusiano kati ya Moscow na mataifa ya Magharibi.

Katika ziara mjini Kyiv mnamo siku ya Jumamosi, viongozi wa Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na Poland waliishinikiza Urusi – wakipata uungwaji mkono wa Trump – kuukubali mpango wa kusitisha mapigano usio na masharti kuanzia leo Jumatatu.

Erdogan yuko tayari kuandaa mazungumzo 

Mkuu wa ofisi ya Rais Zelensky, Andriy Yermak, ameeleza kuwa kiongozi huyo wa Ukraine atakubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo kwa sharti kuwa Moscow nayo itakubali mpango huo wa kusitisha mapigano.

Ikuluu ya Elysee imesema katika taarifa kuwa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameunga mkono wazo hilo, akisisitiza juu ya umuhimu wa kusitisha mapigano kabla ya kufanyika mazungumzo ya aina yoyote.

Katika mkutano wao wa mwisho uliofanyika mjini Istanbul mnamo Machi mwaka 2022, Urusi na Ukraine ziliwasilisha pendekezo la amani ambalo sasa limefutwa, ambalo lingeilazimu Kyiv kuwa na msimamo wa kati na kuachana na mpango wa kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO.

Soma pia: Trump: Zelenskiy yuko tayari kuipa Urusi Crimea

Tangu wakati huo, njia za mawasiliano kati ya Moscow na Kyiv zimekuwa wazi tu linapokuja suala la kubadilisha wafungwa wa vita na miili ya watu waliouwawa.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemwambia Putin kupitia mazungumzo kwa njia ya simu kwamba, Ankara iko tayari kuandaa mazungumzo "yanayolenga kupata suluhisho la kudumu katika mzozo huo.”

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema pendekezo la Urusi la kutaka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja ni "ishara nzuri” ila bado haitoshi, akiishinikiza Moscow kukubali mpango wa kusitisha mapigano.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW