Zelensky aonyesha utayari wa kubadilishana wafungwa na Urusi
13 Januari 2025Pendekezo la Zelensky amelitoa saa chache baada ya idara ya kitaifa ya ujasusi ya Korea Kusini kuthibitisha tangazo la siku iliyopita kwamba Ukraine imewakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini.
Mamlaka nchini Ukraine siku ya Jumamosi ilisema wanajeshi hao wawili walijeruhiwa vibaya katika uwanja wa vita wakati wakipambana na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi, lakini wakati huo hawakutoa ushahidi kuthibitisha uraia wao.
Soma pia: Urusi yadai kuviteka vijiji viwili mashariki mwa Ukraine
Hata hivyo, jana Jumapili, Idara ya ujasusi ya Korea Kusini NIS imeliambia shirika la habari la AFP kwamba, imethibitisha kuwa jeshi la Ukraine limewakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini mnamo Januari 9 katika uwanja wa vita eneo la Kursk, nchini Urusi.
Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini ambao hawataki kurudi nyumbani na wanaoonyesha nia ya kuleta amani kwa kueleza ukweli kuhusu vita hivyo nchini mwao, watapewa kile alichokiita "fursa nyengine."
Alipoulizwa mwaka jana kuhusu ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kaskazini, Rais wa Urusi Vladimir Putin hakukiri wala kukanusha kwamba nchi hiyo inatumia wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Soma pia: Wanajeshi wa Korea Kaskazini wakamatwa na Ukraine
Ukraine, Marekani na Korea Kusini zimeishtumu Korea Kaskazini, nchi yenye silaha za nyuklia kwa kutuma wanajeshi zaidi ya 10,000 kulisaidia jeshi la Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Nchi hizo – Urusi na Korea Kaskazini, zimeimarisha ushirikiano wao wa kijeshi tangu Moscow ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.
Marekani yasema Korea Kaskazini imetuma wanajeshi 10,000 Urusi
Ikulu ya Marekani White House imesema idadi kubwa ya wanajeshi wa Korea Kaskazini wameuawa vitani.
Mnamo mwezi Disemba, shirika la ujasusi la Korea Kusini liliripoti juu wa kukamatwa kwa mwanajeshi wa kwanza wa Korea Kaskazini na vikosi vya Ukraine japo baadaye alifariki dunia.
"Hakuna shaka yoyote duniani kwamba jeshi la Urusi linategemea msaada wa kijeshi kutoka Korea Kaskazini," amesema Zelensky.
Rais huyo wa Ukraine amechapisha video inayoonyesha wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliotekwa wakihojiwa. Mmoja anaonekana amelala kwenye kitanda huku mwengine akiwa ameketi kitandani na bandeji shingoni.