1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky ashinikiza uharakishaji wa kuepeleka silaha Ukraine

17 Februari 2023

Rais wa Ukraine, Volodmyr Zelensky amesema hakuna haja ya mataifa ya Magharibi kuchelewa kuipatia nchi hiyo silaha kwa lengo la kuisadia kupambana na Urusi.

Deutschland | Münchner Sicherheitskonferenz | Wolodymyr Selenskyj
Picha: Johannes Simon/Getty Images

Akizugumza Ijumaa kwa njia ya video katika Mkutano wa Kimataifa wa Usalama unaofanyika mjini Munich, Ujerumani, Zelensky amesema wanahitaji kuharakisha kuisaidia Ukraine, akionya kuwa iwapo mpango huo hautoharakishwa, Urusi itaibuka mshindi katika vita dhidi yake. Amesema kuchelewesha siku zote limekuwa na litaendelea kuwa kosa kubwa.

''Tunahitaji kuharakisha kuyafikia makubaliano, kuharakisha kupeleka silaha na kuharakishi maamuzi ya kudhibiti uwezo wa Urusi,'' alisisitiza Zelensky.

Zelensky: Ukraine sio eneo la mwisho Urusi kuvamia

Zelensky amesema wakati mataifa ya Magharibi yanajadiliana kuhusu kuipatia vifaru Ukraine, Urusi inafikiria njia za kuivamia Moldova na kwamba hakuna njia mbadala ya ushindi wa Ukraine.

Amesema ni wazi Ukraine haitokuwa eneo la mwisho kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin kuvamia, kwani kiongozi huyo ataendelea kwenye mataifa mengine yaliyokuwa katika Muungano wa Kisovieti.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Usalama Munich, UjerumaniPicha: Thomas Kienzle/AFP via Getty Images

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema washirika ambao wanaweza kuipatia Ukraine vifaru vya kivita wafanye hivyo sasa, akisema Ujerumani itawezesha uamuzi huo kwa kutoa msaada wa kimkakati na vifaa, pamoja na kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Ukraine.

Kauli hiyo ameitoa Ijumaa katika mkutano huo wa siku tatu, wakati ambapo washirika wa Jumuia ya Kujihami ya NATO wanajaribu kuipatia Ukraine silaha za kivita.

Ujerumani kuipatia Ukraine vifaru vya Leopard 2

Kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa, mwezi uliopita Ujerumani ilitangaza kuwa itaipatia Ukraine vifaru vya kisasa chapa Leopard 2 kutoka kwenye akiba yake ya jeshi ili kuisaidia nchi hiyo na uvamizi wa Urusi.

Scholz ameuambia mkutano huo wa mwaka unaohudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali takribani 40, wanasiasa, wataalamu wa usalama na wanadiplomasia kutoka kwenye nchi zipatazo 100, kwamba Ujerumani ndiyo inatoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine katika bara la Ulaya. Amesema Ujerumani itaendelea kudumisha usawa kati ya kuisaidia Ukraine na kuepuka kuuzidisha mzozo huo.

Mji wa Bakhmut, UkrainePicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo miwili waandalizi wa mkutano huo hawajawaalika maafisa wa Urusi kutokana na nchi hiyo kuivamia Ukraine Februari 24, 2022.

Brazil kutoipa Ukraine vifaru

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil, Mauro Vieira, amesema nchi hiyo haitoipatia Ukraine vifaru, lakini iko tayari kusaidia kuumaliza mzozo uliopo.

Akizugumza kwenye mkutano huo, Vieira amesema huo ndiyo msimamo wa Brazil, badala ya kushiriki katika vita, wanapendelea kuzungumzia kuhusu amani.

Huku hayo yakijiri katika uwanja wa mapambano, wanajeshi wa Ukraine wanaopambana na vikosi vya Urusi kwenye mji wa Bakhmut wameomba kupatiwa silaha zaidi na mataifa ya kigeni ili kuvisambaratisha vikosi hivyo. Ombi hilo wamelitoa wakati Mkutano wa Usalama Duniani ukiendelea mjini Munich.

 

(AP, AFP, DPA, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW