1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky ataka viongozi wa Urusi wawajibishwe

Josephat Charo
28 Juni 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaita viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Urusi kuwa ni majambazi na kufutilia mbali uwezekano wa mpango wa amani utakaovigeuza vita vya Ukraine kuwa mgogoro uliositishwa.

Ukraine Präsident Selenskyj
Picha: Sergei Supinsky/AFP

Zelensky ametoa kauli hiyo wakati wa hotuba yake mbele ya bunge siku ya katiba ya Ukraine, siku moja baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kuvipongeza vikosi vyake kwa kuudhibiti uasi ulioongzowa na kiongozi wa wapiganaji mamluki wa kampuni ya ulinzi ya Wagner Yevgeny Prigozhin. Zelensky ametangaza kuwa Ukraine iko njiani kuelekea kupata ushindi na kwamba viongozi wa Urusi sharti wawajibishwe kisheria.

"Viongozi wa kisiasa na kijeshi wa shirikisho la Urusi hawatakiwi kukwepa mkono wa sheria kwa sababu wana ulinzi kama viongozi wa dola. Hao si viongozi wa dola. Ni majambazi walioziteka na kuzidhibiti taasisi za dola za Urusi na wakalewa madaraka na hali ya kufanya uhalifu bila hofu ya kuchukuliwa hatua kisheria, na kuanza kuutisha kwa ugaidi ulimwengu wote."

Soma zaidi: Zelensky asema operesheni ya kujibu mapigo inajikokota

Hotuba ya Zelensky imekuja wakati huzuni na simanzi ikitanda katika mji wa Kramatorsk ambako shambulizi la Urusi kwenye mgahawa wa piza lilisababisha vifo vya watu wapatao kumi jana wakiwemo watoto watatu. Watu wengine 58 walijeruhiwa katika hujuma hiyo.

Mgahawa huo ni maarufu sana kwa wanajeshi na waandishi habari katika mji huo ambao ni mojawapo ya miji mikubwa ambayo bado ingali chini ya udhibiti wa Ukraine upande wa mashariki mwa nchi hiyo.

Dmitry Peskov, msemaji wa KremlinPicha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Utawala wa Kremlin mjini Moscow umesema leo kwamba vikosi vya Urusi viliyalenga tu maeneo ya kijeshi nchini Ukraine, kufuatia taarifa za shambulzi hilo dhidi ya mgawaha.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema mashambulizi hufanywa tu dhidi ya vitu ambavyo kwa njia moja ama nyingine vina mafungamano na miundombinu ya kijeshi na wala hawashambulii miundombinu ya kiraia.

Urusi yaukaribisha mpango wa amani wa Vatican

Wakati huo huo utawala wa Kremlin umesema mjumbe wa kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis atafanya mazungumzo na rais Vladimir Putin mjini Moscow wakati Urusi ikiukaribisha mpango wa makao makuu ya kanisa hilo Vatican, wa kutafuta amani katika vita vya Ukraine.

Kadinali Matteo Zuppi alianza ziara yake ya Urusi jana Jumanne na anatarajiwa kuhudhuria misa mjini Moscow kesho jioni.

Soma zaidi: Ukraine yaandaa mkutano wa amani nchini Denmark

Wakati haya yakiarifiwa Uswisi imetanua vikwazo vya kifedha dhidi ya taasisi na raia wa Urusi kulingana na vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya serikali ya mjini Mowcow, kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine.

Miongoni mwa wanaolengwa katika vikwazo hivyo ni watu, makampuni na mashirika yanayosaidia mchakato usio halali wa kuwasafirisha watoto wa Ukraine kwenda Urusi.

Vinawajumuisha pia maafisa wa majeshi ya Urusi, wawakilishi wa ngazi za juu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi na wanachma wa kampuni ya wapiganaji mamluki ya Wagner.

Vikwazo hivyo vinahusu kuzuiwa kwa mali na marufuku ya kusafiri kwenda au kupitia Uswisi.

(afp, reuters)