Zelensky awasili London kwa mazungumzo na kiongozi wa UK
17 Machi 2026
Rais Zelenskyy atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu Keir Starmer, kwa mujibu wa serikali ya Uingereza, wakati nchi za Ulaya zikijaribu kuendeleza mkazo wa kimataifa kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, huku vita vinavyoendelea kati ya Iran na mataifa ya Magharibi vikiwavuta viongozi wa dunia.
Ofisi ya Starmer ilisema kwamba Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte pia atahudhuria kikao hicho katika makazi ya waziri mkuu kujadili juhudi za kuleta amani nchini Ukraine na "umuhimu wa kuendeleza shinikizo la vikwazo dhidi ya Urusi.”
Mkutano huo unafanyika siku chache baada ya Marekani kulegeza kwa muda baadhi ya vikwazo vya mafuta ya Urusi ili kupunguza shinikizo katika masoko ya mafuta duniani lililosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati, ambavyo vilizuka kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanzia Februari 28.
Zelenskyy aliikosoa hatua ya Washington ya kulegeza vikwazo, akisema kuwa itatoa fursa kwa Moscow kupata mapato makubwa zaidi na kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.
Mazungumzo yanayoongozwa na Marekani kati ya wajumbe wa Moscow na Kyiv, ambayo hadi sasa hayajazaa matunda katika masuala muhimu, yamepoteza kasi kutokana na mgogoro unaondelea Mashariki ya Kati. Kutoka Uingereza, Zelensky ataelekea Uhispania siku ya jumatano. Akizungumza na shirika la habari la Reuters, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amesema linapokuja suala la mazungumzo na Urusi, Ulaya inapaswa kuwa mwangalifu.
"Na tunapozungumza na Urusi, bila shaka, jambo la muhimu zaidi ni kukubaliana kwanza, tunataka kuzungumza nao nini. Kwa sababu tukirejea tu katika hali ya kawaida kama ilivyokuwa hapo awali, tutapata mambo yale yale—vita zaidi. Tumeliona hili awali, kwa hiyo tunapaswa kuwa waangalifu sana na tusiwape Urusi kile wanachotaka, kwa sababu matamanio yao yatazidi tu kuongezeka.”
Urusi yashambulia miundombinu ya nishati, bandari na viwanda
Wakati hayo yakiendelea,shambulizi la usiku kucha la Urusi limeharibu miundombinu ya viwanda, bandari na nishati katika mkoa wa Ukraine wa Odesa ulioko katika Bahari Nyeusi na kutatiza ugavi wa umeme katika maeneo ya kusini ya mkoa huo.
Gavana wa mkoa huo Oleh Kiper amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba moto uliosababishwa na shambulizi hilo umedhibitiwa na hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Gavana wa mkoa mwingine wa Izmail ambao uko na bandari kubwa katika mto Danube karibu na nchi mwanachama wa jumuiya ya kujihami NATO Romania, alisema kuwa umeshambuliwa kwa droni usiku kucha na kuharibu miundombinu ya usafiri na majengo ya makaazi.
Wizara ya ulinzi ya Romania ilisema katika taarifa yake Jumanne, kwamba ilikuwa ikifuatilia mabaki ya vipande vya Droni vinavyodaiwa kuangukia karibu na kijiji kimoja kando ya mto Danube baada ya shambulio hilo.
Aidha pia, vikosi vya Urusi vinaripotiwa kuchukua udhibiti wa vijiji viwili katika mji wa kaskazini mwa Ukraine wa Summy na mkoa wa mashariki wa Donetsk. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema pia kwamba ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita, wamezidungua ndege za droni zaidi ya 400 zilizorushwa na Ukraine.
EU ijiandae kwa mazungumzo na Urusi
Na mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya Antonio Costa, amesema muungano huo unapaswa kujiandaa kwa mazungumzo na Urusi. Costa ameeleza kwamba kwa hivi sasa, EU haitakiwi kuingilia juhudi zinazofanywa na rais wa Marekani Donald Trump kutafuta amani ya Ukraine.
Lakini ameongeza kwamba, endapo mazungumzo hayo yatashindwa kuendelea au kuvunjika, basi Umoja wa Ulaya ujiandae kuendeleza juhudi hizo za kusaka amani ya kudumu kwa ajili ya Ukraine.