1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Zelensky awasili Paris kuongeza msukumo dhidi ya Urusi

13 Machi 2026

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasili mjini Paris hii leo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron kuhusu njia za kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Urusi.

Ufaransa Paris 2025 | Mkutano kati ya Emmanuel Macron na Volodymyr Zelensky
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimkaribisha mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya ÉlyséePicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Ziara hiyo inafanyika wakati mazungumzo ya kusitisha vita vya miaka minne na ambayo yalikuwa yakiongozwa na Marekani, yamekwama kutokana na mzozo mpya unaoendelea kufukuta kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. 

Msemaji wa Zelensky, Sergiy Nykyforov, amewaambia waandishi wa habari kuwa viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana leo mchana na baadaye kufanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Hii ni ziara ya 12 ya Zelensky nchini Ufaransa tangu vita kati ya nchi yake na Urusi vilipoanza mnamo mwaka 2022.

Mapema wiki hii, Ikulu ya Kremlin iliukosoa mkutano huo, ikidai kuwa utavuruga mchakato wa amani unaoendelea. Serikali ya Urusi ilisema kuwa "jaribio lolote la kuiwekea shinikizo Urusi ni la kipuuzi," ikionyesha kutoridhishwa na hatua za mataifa ya Magharibi.

Mazungumzo kati ya Macron na Zelensky yanatarajiwa kujikita katika kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi, hususan kwa kulenga msafara wa siri wa meli za mafuta, unaotumiwa na Moscow kusafirisha mafuta kwa kukwepa vikwazo vya kimataifa. Meli hizo zimekuwa njia muhimu kwa Urusi kuendelea kuuza mafuta licha ya vikwazo.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema wiki hii kwamba baadhi ya vikwazo vya mafuta vitaondolewa kama sehemu ya kudhibiti bei ya mafuta katika soko la kimataifa. Ingawa hakutaja nchi maalum, hatua hiyo inakuja baada ya utawala wake kuashiria uwezekano wa kulegeza masharti ya mauzo ya mafuta ya Urusi.

Serikali ya Marekani pia imeamua kupunguza kwa muda baadhi ya vikwazo vya kiuchumi ili kuruhusu mafuta ya Urusi yaliyokwama baharini kuuzwa kwa India hadi tarehe 3 Aprili.

Zelensky na Romania waafikiana kutengeneza droni

Kabla ya kuwasili Paris, Zelensky aliitembelea Romania ambako alijadiliana na viongozi wa Bucharest kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi.

Pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha utengenezeji wa pamoja wa droni ili kuongeza uwezo wa Ukraine katika vita vyake na Urusi.

"Nchi yoyote barani Ulaya inaweza kujikuta ikikabiliwa na tishio. Ndio maana mfumo wa pamoja ambao Ukraine imeujenga kwa juhudi kubwa sasa utaanza kufanya kazi katika ngazi ya wataalamu, pamoja na washirika wetu wa Mashariki ya Kati na Marekani. Na ninaamini ni muhimu kuendeleza hatua hizi kwa ushirikiano na nchi za Ulaya—majirani zetu na marafiki wetu," alisema Zelensky.

Mtaalam wa droni kutoka kampuni ya Ukraine ya General Cherry akionyesha jinsi droni zinavyofanya kazi kudhibiti mashambulizi ya anga ya Urusi Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Ziara ya Zelensky nchini Ufaransa inafanyika wakati Hungary, mwanachama wa Umoja wa Ulaya, imezuia mkopo muhimu wa euro bilioni 90 sawa na dola bilioni 106 kwa Ukraine. Budapest pia imepinga duru mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi.

Hungary na Slovakia zimeishutumu Ukraine kwa kuchelewesha kufunguliwa kwa bomba la mafuta la Druzhba, ambalo husafirisha mafuta ya Urusi kwenda katika nchi hizo mbili zisizo na bandari. Ukraine imekanusha shutuma hizo, ikisema bomba hilo liliharibiwa na mashambulizi ya Urusi mwezi Januari.

Umoja wa Ulaya ilieleza jana Alhamisi kuwa imependekeza kutuma timu maalum ya kukagua bomba hilo na ilikuwa inasubiri majibu kutoka Kyiv. Zelensky alisema wiki iliyopita kuwa ukarabati wa bomba hilo unaweza kuchukua kati ya wiki nne hadi sita kabla ya kuanza tena kusafirisha mafuta.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW