1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky awataka raia wa Ukraine kuendelea na mapambano

22 Machi 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewatolea mwito raia wa nchi hiyo kuendelea na mapambano dhidi ya wanajeshi wa Urusi katikati ya ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia.

Ukraine-Konflikt - Selenskyj in Kiew
Picha: Uncredited/Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture-alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewapongeza waandamanaji katika mji unaokaliwa kimabavu wa Kherson, kwa ujasiri wao wa kukabiliana na wanajeshi wa Urusi waliofyatua risasi kutawanya maandamano hayo.

Akizungumza kwa njia ya video, Zelensky amesema wameona "watumwa wakifyatua risasi kwa watu walio huru na kuwataja wanajeshi wa Urusi kama watumwa wa propaganda."

Soma pia: Mapigano ya kuwania Mariupol yapamba moto Ukraine

Rais huyo wa Ukraine ameongeza kuwa, vita hivyo vimewageuza raia wa kawaida wa Ukraine kuwa mashujaa na kwamba ushujaa huo pia umewashangaza "maadui".

Jeshi la Urusi lafyatua risasi hewani kuzima maandamano

Raia wa Ukraine waandamana kupinga kuchukuliwa kimabavu mji wa KhersonPicha: Yanis Obarchuk

Wanajeshi wa Urusi jana Jumatatu walitumia mabomu na kufyatua risasi hewani ili kuzima maandamano katika mji wa kusini wa Kherson. Waandamanaji hao wanapinga hatua ya kuchukuliwa kwa nguvu mji huo wa kusini mwa Ukraine baada ya uvamizi wa mwezi uliopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alichapisha video kwenye mtandao wa Twitter, ikimuonyesha mwanamume aliyebeba bendera ya Ukraine aliyejeruhiwa kwa risasi. Kwenye video hiyo, milio ya risasi inasikika na kuonyesha watu waliobeba bendera wakikimbia ili kumsaidia mwanamume huyo aliyekuwa akivuja damu.

Soma zaidi:Rais Zelenskiy ataka mazungumzo ya kina na Moscowi: 

Kherson, mji wenye takriban watu 200,000 upo karibu na rasi ya Crimea, iliyotwaliwa na Urusi mwaka 2014 na ni mojawapo ya njia zilizotumika na Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi uliopita.

Mji huo ulikuwa wa kwanza kuingia mikononi mwa vikosi vya usalama vya Urusi, huku Moscow ukiuteka mji huo ndani ya wiki ya kwanza ya uvamizi wake nchini Ukraine. Watu wa mji huo hata hivyo wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara kupinga kuchukuliwa kwa nguvu mji huo wa kusini.

Vyombo vya habari nchini Ukraine vimeripoti mara kadhaa kuwa vikosi vya usalama vya Urusi vimekuwa vikiwafyatulia risasi waandamanaji.

Ukraine inadai jeshi la Urusi limekamata raia 400 katika mji wa Kherson

Picha: via REUTERS

Mapema mwezi huu, mamlaka nchini Ukraine ilisema wanachama wa jeshi la ulinzi wa kitaifa wa Urusi wamewaweka kizuizini zaidi ya watu 400 katika mji huo wa Kherson.

Wakati hayo yakiarifiwa, shirika la habari la Interfax limeripoti kuwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mkutano na Rais wa Urusi Vladimir Putin ni muhimu katika kumaliza vita nchini Ukraine.

Wa-Ukraine waapa kutetea maeneo yao

02:15

This browser does not support the video element.

Shirika hilo la habari la Interfax limemnukuu Zelensky akitoa kauli hiyo katika mahojiano ya runinga.

Zelensky ametoa wito kwa Ulaya kuongeza mbinyo kwa Urusi ili kusitisha vita hivyo, akitaka mataifa ya Ulaya kukata kabisa biashara na Urusi.

Ama kwa upande mwengine, viongozi wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia wamefanya tena mazungumzo ya dharura juu ya vita hivyo.

Rais Joe Biden na washirika wa Ulaya walizungumza kwa njia ya simu, mazungumzo yaliyodumu chini ya saa moja na Rais Emmanuel Macron, Kansela Olaf Scholz, Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kujadili juu ya kadhia hiyo.

Pia, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamekutana mjini Brussels kujadili juu ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi.