1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky azitembelea Berlin, Paris kusaka msaada zaidi

16 Februari 2024

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine anafanya ziara nchini Ujerumani na Ufaransa, ambako anatarajiwa kutia saini mikataba ya usalama na kutafuta uungwaji mkono zaidi katika vita vya Kyiv dhidi ya Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Picha: president.gov.ua

Haya yanajiri huku Ukraine ikisema kwamba kumekuwa na mapigano makali katika mji wa Avdiivka ambao umekuwa shabaha kuu ya Urusi wakati vita hivyo vikikaribia kuingia mwaka wa tatu. 

Soma pia: Hali ngumu kwa wanajeshi wa Ukraine walioko mashariki

Zelensky anatarajiwa kuwasilisha ombi lake la msaada endelevu wa ufadhili na silaha kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich, ambapo viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris wanatarajiwa kuhudhuria.

Ziara ya Zelensky barani Ulaya inajiri katika wakati muhimu kwa wanajeshi wa Ukraine, ambao wanakabiliwa na hali ngumu zaidi kwenye uwanja wa mapambano upande wa mashariki kutokana na uhaba wa silaha na mashambulio mapya ya Urusi.

Kabla ya kuanza ziara yake kuelekea Berlin na Paris rais Zelensky alisema kwamba kuna mikakati ya kuunda "usanifu mpya wa usalama" nchini Ukraine.

Zelensky alisema "Mikutano muhimu na washirika imepangwa. Kutakuwa na makubaliano mapya. Tunafanya kila tunachoweza ili kuwe na ufanisi kwa Ukraine, na nina hakika itakuwa hivyo.

"Tunaunda usanifu mpya wa usalama wa nchi yetu ambao utatusaidia sio tu hapa na sasa, lakini kwa muda mrefu. Na hili ni jambo ambalo Ukraine haijawahi kuwa nalo, ingawa imekuwa ikihitaji siku zote." aliongezea Zelensky.

Mkwamo wa ufadhili

Rais Joe Biden wa Marekani akilihutubia bunge.Picha: Victoria Spartz/Getty Images

Mustakabali wa muda mrefu wa mabilioni ya dola ya msaada wa nchi za Magharibi uko mashakani, huku mchangiaji mkuu, Marekani, akiwa katika hekaheka za mwaka wa uchaguzi. Msaada wa kijeshi wa takriban dola bilioni 60 umezuiliwa huko Washington tangu mwaka jana kwa sababu ya mabishano katika bunge la Marekani.

Pigo jengine kwa Ukraine ni kwamba Umoja wa Ulaya, umekiri unaweza tu kuchangia nusu ya makombora milioni moja iliyoahidi kutuma ifikapo mwezi Machi.

Soma pia: Umoja wa Ulaya kulazimika kuiongezea msaada Ukraine

Katika uwanja wa mapambano, Ikulu ya White House imeonya kwamba Jeshi la Urusi liko mbioni kuuteka mji wa mashariki mwa Ukraine wa Avdiivka, baada ya miezi kadhaa ya mapigano.

Kupitia mtandao wa kijamii jenerali wa Ukraine katika upande wa mashariki, Oleksandr Tarnavskiy, ameandika kwamba "Vita vikali vinaendelea ndani ya jiji, na kuitaja hali katika mji wa Avdiivka kuwa ni "ngumu lakini iliyodhibitiwa" na kwamba makamanda wa Ukraine wamepewa jukumu la "kutuliza hali."

Kwa upande wa Urusi shirika la habari la TASS limeripoti kwamba, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilitangaza kuwa droni moja ilidunguliwa na walinzi wa anga wa Urusi katika eneo la kusini-magharibi mwa Urusi katika mkoa wa Belgorod karibu na mpaka na Ukraine na droni nyengine nne katika Bahari Nyeusi.

 

//AFP, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW