Zelensky: Crimea lazima irejee chini ya uthibiti wa Ukraine
8 Aprili 2023Katika ujumbe kupitia video iliyochapishwa na ofisi yake, Zelensky amesema kuwa dunia inapaswa kufahamu kwamba heshima na utaratibu vitarejea tu katika uhusiano wa kimataifa wakati bendera ya Ukraine itakapopeperushwa tena katika eneo hilo la Crimea.
Zelensky asema kukombolewa kwa Crimea ni kwa manufaa ya kimataifa
Katika video tofauti iliyonakili mkutano kati yake na wanajeshi wa kiislamu waliowajumuisha wawakilishi wa jamii ya Kituruki katika eneo hilo, Zelensky amesema kuwa kukombolewa kwa Crimea sio tu muhimu kwa Ukraine, lakini pia kwa dunia nzima na anaamini hilo. Jamii hiyo ya Waturuki wa Crimea ni jamii ya waislamu wachache ambao ni wazawa wa rasi ya Crimea. Wengi wao wametoroka eneo hilo kwa hofu ya mateso ya kisiasa na wengine wako chini ya vizuizi vya Urusi.
Rais wa Brazil aitaka Ukraine kuiachilia Crimea
Matamshi ya Zelensky yanakuja baada ya rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva kupendekeza kwamba Ukraine iachilie eneo hilo la Crimea, ambalo Urusi ililiteka kimabavu mnamo mwaka 2014 kama sehemu ya uwezekano wa makubaliano ya amani na Urusi. Pendekezo hilo pia liligusiwa wiki hii na mshirika wa timu ya Zelensky mwenyewe.
Mazungumzo kuhusu Crimea kufanyika kwa masharti
Naibu mkuu wa ofisi ya Zelensky, Andriy Sybiha, ameliambia gazeti la Financial Times kwamba huenda Ukraine ikawa wazi kwa mazungumzo kuhusu Crimea ikiwa mashambulizi yanayotarajiwa ya msimu wa machipuko yatathibitisha kufanikiwa. Sybiha ameongeza kuwa ikiwa watafanikiwa kuafikia malengo yao ya kimkakati katika uwanja wa vita na wakati watakapokuwa kwenye mpaka wa kiutawala na Crimea, basi watakuwa tayari kuanzisha mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu suala hilo.