1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky kuomba msaada tena Umoja wa Ulaya

9 Februari 2023

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels umemualika rais Zelensky kushiriki mkutano huo na kulihutubia bunge la Umoja wa Ulaya

Belgien Brüssel | EU-Gipfel | Wolodymyr Selenskyj und Roberta Metsola
Picha: Kenzo Tribouillard/AFP

Mjini Brussels leo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwenye mkutano wao wa kilele na rais wa Ukraine Volodymry Zelensky amealikwa kushiriki mkutano huo.

Atalihutubia bunge la Umoja wa Ulaya akitarajiwa  kuwatolea mwito viongozi hao kuipatia nchi yake madege ya kivita na silaha nyingine zaidi kujiimarisha kiulinzi dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Rais Zelensky amewasili Brussels ambako ni makao makuu ya Umoja wa Ulaya,akitokea Paris na Uingereza alikokuweko jana Jumatano.

Mjini Paris Ufaransa alifanya mazungumzo pamoja na rais Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na baadae wote wakazungumza na waandishi habari.Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimuhakikishia kiongozi huyo wa Ukraine kwamba Ufaransa na Umoja wa Ulaya wako  pamoja nae.

''Ukraine inaweza kuitegemea Ufaransa na washirika wake Umoja wa Ulaya na washirika  wengine kushinda vita hivi. Urusi haiwezi na haipaswi kushinda.''

Rais Zelensky anatarajiwa kuwatolea mwito viongozi wa Umoja wa Ulaya kuongeza msaada kwa nchi yake inayozongwa na vita vinavyoendeshwa na Urusi. Viongozi mbali mbali wa nchi na serikali kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya wako Brussels na baadhi wameshazungumza na kutowa mwelekeo wa kinachotarajiwa.

Akiwasili kwenye mkutano huo Kansela wa Ujerumani Olafa Scholz amesisitiza juu ya msaada wa nchi yake kwa Ukraine akisema Ujerumani ndio nchi ya Umoja wa Ulaya inayotowa kiwango kikubwa msaada wa fedha na kibinadamu kwa Ukraine lakini pia ndiyo yenye uungaji mkono wa dhati linapokuja suala la kupeleka silaha nchini humo.

Picha: Yves Herman/REUTERS

Kansela Scholz pia ameongeza kusema kwamba kualikwa Zelensky kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya ni alama ya kuonesha umoja na  mshikamano kwa mara nyingine na kuonesha kwamba Umoja huo utaendelea kuiunga mkono Ukraine katika kutetea uhuru na uthabiti wake.Baada ya Uingereza, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akutana na Macron, Scholz mjini Paris

Rais wa Baraza la ulaya Charle Michel amesema ni muhimu kuongeza msaada kwa Ukraine. Waziri mkuu wa Estonia  Kaja Kallas baada ya kuwasili Brussels nae ameweka wazi kwamba  ni muhimu kuharakisha msaada wa kijeshi kuelekea Ukraine na hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa.

Nchi zenye nguvu katika Jumuiya ya kujihami ya NATO na kwenye Umoja wa Ulaya sambamba na Marekanoi zimekuwa ndio waungaji mkono wakubwa wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine  tangu Urusi ilipoanzisha vita kamili ya uvamizi dhidi ya nchi hiyo.

Picha: Bogdan Hoyaux/EC

Na kwahivyo viongozi wa Umoja wa Ulaya leo wanatarajiwa pia kusifu hatua waliyochukua ya kutumia euro bilioni 67 kuisadia kijeshi na kifedha Ukraine ikiwemo fedha zilizotumika kuwapokea wakimbizi milioni 4 kutoka Ukraine.

Japo rais Zelensky anatazamiwa vile vile kuomba msaada zaidi ,kwasababu Jeshi la nchi yake linakabiliwa na mashambulizi mapya ya Urusi na makamanda wake wanahitaji madege ya kisasa kabisa ya kivita kutoka nchi za Magharibi ili kuilinda anga yake dhidi ya Urusi.