1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Kurejea kwa Trump ni ukurasa mpya kwa dunia

Hawa Bihoga
9 Januari 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House kutaleta "ukurasa mpya" kwa siasa za kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuishinikiza Urusi kufanikisha amani.

Ukraine | Rais Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Sergei Supinsky/AFP/ Getty Images

Rais Zelensky ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa washirika wa Ukraine wapatao 50 uliofanyika katika kambi ya anga ya Marekani ya Ramstein, iliyoko nchini Ujerumani.

Mkutano huo, unaotarajiwa kuwa wa mwisho wa aina yake kabla ya Donald Trump kuchukua madaraka mnamo Januari 20, umeibua maswali kuhusu mustakabali wa msaada wa Marekani kwa Kyiv. 

Katika hotuba yake, Zelensky ameonyesha wasiwasi kuhusu uungaji mkono wa siku zijazo na akaendelea kusisitiza wito wake kwa washirika wa Magharibi kupeleka vikosi vya kijeshi.

Soma pia:Jeshi la Ukraine limesema limedungua droni 41 dhidi ya Ukraine

Alisema kuwa hatua hiyo inaweza kuwa njia bora ya kuilazimisha Urusi kuingia kwenye makubaliano ya amani, hasa wakati ambapo vita hivyo vinaelekea mwaka wake wa tatu.

''Lengo la Putin halijabadilika. Anataka kuiharibu Ukraine kabisa — na pia kutuvunja nguvu sisi sote, pamoja na ninyi. Ndiyo maana lengo letu ni kupata njia nyingi iwezekanavyo za kuilazimisha Urusi kukubali amani.

Aliongeza kwamba kwamba "kupelekwa kwa vikosi vya washirika ni moja ya njia bora zaidi. Hebu tuwe wa vitendo zaidi katika kuhakikisha hili linawezekana.''

Marekani yaongeza msaada zaidi kwa Kyiv

Marekani chini ya Rais Joe Biden imekuwa mshirika mkubwa wa Ukraine wakati wa vita, ikitoa msaada wa kijeshi wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 65 tangu Februari 2022.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, ametangaza msaada mpya wa kijeshi wa dola milioni 500 kwa Kyiv, akisisitiza kuwa vita vya Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi vinawahusu wote.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

02:30

This browser does not support the video element.

''Kwa hivyo hatupaswi kulegeza kamba, na ndiyo maana leo natangaza awamu nyingine ya msaada wa rais wenye thamani ya dola milioni 500."

Alisema msaada huo unajumuisha makombora ya ziada kwa ajili ya ulinzi wa anga wa Ukraine, risasi zaidi, mifumo ya mashambulizi angani, na vifaa vingine vya kusaidia ndege za kivita za Ukraine chapa F-16.

Donald Trump ameahidi kuvimaliza vita vya Ukraine haraka bila kutoa mpango mahsusi, huku mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, akisema umoja huo uko tayari kuchukua uongozi endapo Marekani itapunguza msaada wake. Amesisitiza kuwa si kwa maslahi ya Marekani kuruhusu Urusi kuwa na nguvu kubwa zaidi duniani.

Soma pia:Katibu Mkuu wa NATO kumshawishi Trump juu ya mkataba wa silaha

Vikosi vya Urusi na Ukraine vinaendelea kupambana vikali wakijaribu kuimarisha nafasi zao za kivita kabla ya Trump kuapishwa.

Trump ameikosoa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa kutumia bajeti kidogo kwenye ulinzi wa pamoja, na wiki hii alizusha wasiwasi zaidi kwa kukataka kuondoa uwezekano wa kuichukua kwa nguvu za kijeshi Greenland, ambayo ni eneo linalojitegemea la Denmark, mwanachama wa Umoja wa Ulaya na NATO.

Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema washirika wanapaswa kuisaidia Ukraine kufikia nafasi ya nguvu kabla ya makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano au mazungumzo ya amani. 

Amesema kuwa baada ya mazungumzo hayo kumalizika, itapimwa kama ni makubaliano mazuri au la, kwani dunia nzima, ikiwa ni pamoja na China, Korea Kaskazini, Iran, na Urusi, inafuatilia kwa karibu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW