Zelensky: Mazungumzo ya Kiev na Moscow kuendelea Abu Dhabi
2 Machi 2026
Hata hivyo, Zelenskiy amesema Ukraine inazingatia uwezekano wa kubadili eneo la mkutano huo kutokana na hali ya usalama. Amesema Uturuki au Uswisi zinaweza kuwa chaguo mbadala iwapo hali haitaruhusu kufanyika kwa mkutano katika Falme za Kiarabu. Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Zelenskiy alisema:
Ikiwa kufanya mkutano Abu Dhabi itakuwa vigumu kwa sababu ya mashambulizi ya makombora na droni, basi naamini bado tunaweza kuwa na Uturu na Uswisi, maeneo ambayo tayari yamefanyika na kumuwezesha kila moja kukutana. Tutaunga mkono lolote kati ya maeneo hayo matatu. Tunasubiri jibu kutoka kwa washirika wetu.
Kwa upande wake, Kremlin imesema ni kwa maslahi ya Urusi kuendelea na mazungumzo hayo. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema Moscow inapendelea suluhisho la kisiasa na kidiplomasia kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka minne sasa.
Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekwama katika wiki za karibuni kutokana na msimamo wa Urusi kuitaka Ukraine ikabidhi sehemu iliyobaki ya eneo la Donbas mashariki, ambalo Moscow haijaliteka kikamilifu. Zelenskiy amesisitiza mara kwa mara kuwa hatakubali kuachia takribani asilimia 20 ya eneo la Donetsk ambalo bado liko chini ya udhibiti wa Ukraine.
Zelensky: Urusi inajiandaa kwa wimbi jipya la mashambulizi
Rais huyo wa Ukraine amesema msimamo wa nchi yake umeimarika baada ya kustahimili kipindi kigumu cha majira ya baridi na mashambulizi makali ya droni na makombora ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati. Amesema Ukraine itaendelea kujilinda na haitasalimu amri kwa masharti yanayolazimishwa.
Zelenskiy pia ameeleza kuwa hadi sasa mapigano ya Mashariki ya Kati hayajaathiri usambazaji wa silaha kutoka kwa washirika wa Ukraine. Hata hivyo, ameonya kuwa iwapo vita vitaendelea kwa muda mrefu na mashambulizi kuongezeka, kiwango cha vifaa vya ulinzi wa anga kinachopatikana kinaweza kuathirika.
Amesema Urusi inajiandaa kwa wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya miundombinu, vifaa vya usafirishaji na hata huduma za maji. Hivyo, kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa mifumo ya ulinzi wa anga bado ni changamoto kubwa kwa Kyiv.
Wakati huo huo, Zelenskiy amesema Ukraine iko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya kiufundi kwa ajili ya kufungua mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Amewahimiza washirika wa EU kuweka tarehe rasmi ya uanachama, akisema hilo ni muhimu kama sehemu ya dhamana za usalama katika mazungumzo ya kumaliza vita.