1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Mji wa Soledar bado haujakamatwa na Urusi

12 Januari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mapigano bado yanaendelea kwenye mji muhimu wa mashariki mwa nchi hiyo wa Soledar ambao mamluki wa kundi binafsi la ulinzi kutoka Urusi la Wagner walisema wameukamata.

Ukraine-Krieg | Kämpfe um Soledar
Mapambano ya kuwania mji wa Soledar Picha: Libkos/AP/dpa/picture alliance

Kupitia ujumbe wa vidio anaoutoa kila siku kwa taifa, rais Zelensky amesema Urusi na washirika wake wanajaribu kufanya propaganda kwa madai ya kuukamata mji wa Soledar lakini ukweli ni kwamba  mapambano bado yanaendelea. Amesema vikosi vya nchi yake vilivyo mstari wa mbele bado vimesimama imara kudhibiti hujuma za "maadui".

Hatma ya mji huo ulio kwenye mkoa wa Donetsk na unaofahamika kwa uzalishaji mkubwa wa chumvi bado haijulikani tangu kundi la Wagner liliporipoti kuwa limechukua udhibiti wa njia muhimu kuingia kwenye mji huo.

Hadi sasa pande zote mbili yaan Urusi na Ukraine zimesema mapigano ya kuwania udhibiti wa mji huo ni makali na yamechukua muda mrefu na Moscow imetahadharisha madai ya ushindi wa mapema yanayotolewa na kundi la Wagner.

Mji wa Soledar unapatikana kiasi maili tisa kutoka mji mwingine wa Bakhmut ambao vikosi vya Urusi vimekuwa vikijaribu pia kuukamata.

Zelensky apokea msaada wa kijeshi kutoka Poland na Lithuania

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine Picha: President of Ukraine/apaimages/IMAGO

Mbali ya suala la mji wa Soledar, rais Volodymyr Zelensky alitumia hotuba yake ya jana usiku kuwashukuru viongozi wa Poland na Lithuania kwa kutuma awamu nyingine ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Msaada huo unaojumuisha vifaru mamboleo aina ya Leopard kutoka Poland na mfumo wa kujilinda na makombora kutoka Lithuania ulitangazwa baada ya Zelensky kukukatana na viogozi wa mataifa hayo mawili kwenye mji wa Lviv.

Zelenksy amesema zana zote hizo hizo "tunazihitaji kujilinda na ndege zisizo rubani za Iran na kulinda sekta yetu ya nishati".

Moscow yabadili kamanda wa vikosi vyake Ukraine 

Wakati hayo yakiendelea upande wa Ukraine, Urusi kwa upande wake imemtangaza jenerali mpya kuongoza mzozo wa Ukraine.

Wizara ya Ulinzi mjini Moscow imesema mkuu wa utumishi wa jeshi la Urusi Valery Gerasimov ndiye atabeba jukumu la kile inakiita operesheni maalumu nchini Ukraine.

Kamanda Sergei Surovikin aliyekuwa mkuu wa vikosi vya Urusi nchini Ukraine amebadilishwa.Picha: Sergei Bobylev/Tass/dpa/picture alliance

Aliyekuwa na jukumu hilo hadi jana Jumatano Jenerali  Sergei Surovikin atachukua nafasi naibu mkuu wa vikosi vya Urusi huko Ukraine. Hakuna sababu au maelezo ya ziada yaliyotolewa juu ya uamuzi wa kufanyika mabadiliko hayo.

Katika hatua nyingine afisa wa Marekani amesema mapato ya Urusi yatokanayo na biashara ya mafuta yanapungua tangu mataifa ya magharibi yalipotangaza ukomo wa bei kwa nishati hiyo kutoka Moscow.

Afisa huyo mwandamizi kwenye wizara ya fedha ya Marekani amesema Urusi inapoteza mabilioni ya fedha kila siku kutoka na ukomo wa bei wa dola 60 kwa pipa uliofikiwa na mataifa ya kundi la G7, Umoja wa Ulaya na Australia mwaka uliopita.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW