Zelensky na viongozi wengine wahutubia UNGA-80
24 Septemba 2025
Katika siku hii ya pili ya Mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, viongozi waliohutubia Jumatano ni pamoja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, rais wa Iran Masoud Pezeshkian na yule wa Syria Ahmed al-Sharaa. Mjadala huo umepangwa kuendelea hadi Jumatatu ambapo jumla ya wakuu wa nchi na serikali wapatao 150 na wawakilishi wengine wa kitaifa wakitarajiwa kutoa hotuba zao.
Katika hotuba yake, Zelensky amesema uhalisia wa sasa wa dunia unaonyesha kuwa ili nchi yoyote iweze kuishi kwa kuwa na hakikisho la usalama ni lazima iwe na washirika imara na silaha. Amelaumu pia mfumo wa Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua za kumaliza vita katika nchi yake ya Ukraine, Somalia na kwengineko akisema taasisi hiyo imebaki tu ya kutoa matamko yasiyosaidia chochote.
Mfalme wa Uhispania Don Filipe VI amehutubia pia leo katika mkutano huu unaoadhimisha miaka 80 ya Umoja wa Mataifa na kuitaka jamii ya kimataifa kuzingatia sheria, haki na usawa na kusisitiza kuwa vitu hivyo ni muhimu hasa katika nyakati hizi ambazo dunia inakabiliwa na mizozo kama vita vya Ukraine na huko Mashariki ya Kati .
Teknolojia ya akili mnemba kujadiliwa pia
Zaidi ya hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kujadili mada ya teknolojia ya akili mnemba katika wakati ambapo watu karibu 200 wakiwemo wataalam wa masuala ya teknolojia, wanasiasa na washindi wa Tuzo ya Nobel wakitoa wito kwa mataifa kote ulimwenguni kuchukua hatua za kudhibiti matumizi ya akili mnemba.
Katika kikao kilichopita cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa watu hao walisaini nyaraka ya pamoja na kueleza kuwa akili mnemba "AI" ina uwezo mkubwa wa kuendeleza ustawi wa binaadamu, lakini mwelekeo wake wa sasa unadhihirisha hatari ambazo hazijawahi kushuhudiwa, wakitoa wito kwa serikali zote duniani kuchukua hatua madhubuti kabla hali haijawa mbaya zaidi na isiyodhibitiwa.
Kundi la watu hao limehimiza kuwepo na sheria za kimataifa za kudhibiti teknolojia ya akili mnemba hasa kwa matumizi yatakayodhihirika kuwa hatari mfano matumizi ya teknolojia hiyo ya AI katika miundombinu ya silaha za nyuklia au aina yoyote ya mfumo hatari wa silaha. Mifano mingine iliyotolewa ni kuiruhusu AI kutumiwa katika vitendo vya kuwachunguza watu wengi, kughushi taarifa za mtu au hata mashambulizi ya mtandaoni.
// AP, AFP