1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Urusi imeshambulia hospitali na vituo vya matibabu

6 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksyy amesema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za matibabu na dawa katika maeneo ya mashariki na kusini yanayodhibitiwa na Urusi nchini Ukraine.

Standbild aus DW TV-Bericht "Zelenskyy says ceasefire is vital for Mariupol evacuation"
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyyPicha: Ukrainian Presidency/AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa oparesheni ya tatu ya kuwahamisha raia kutoka mji wa bandari wa Mariupol na kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichozingirwa inaendelea, wakati Urusi ikishtumu nchi za Magharibi kwa kuendesha vita vya dunia vya kiuchumi.

Katika mkutano na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres alikataa kutoa maelezo juu ya oparesheni hiyo mpya "ili kuepusha uwezekano wa oparesheni hiyo kuvurugwa." Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Shirika la msalaba mwekundu ICRC, hadi sasa yamewaokoa karibu watu 500 kutoka Mariupol katika muda wa wiki moja iliyopita.

Soma pia: Vita vya Ukraine: Urusi yaendeleza mashambulizi katika kiwanda cha chuma cha Azovstal

Guterres amesema, "Natumai maelewano kati ya Moscow na Kyiv kutatoa fursa zaidi ya njia salama kuruhusu raia kuondoka katika maeneo ya mapigano na misaada kuwafikia wahitaji. Lazima tufanye kila linalowezekana kuwaokoa watu hao wanaokabiliwa na mazingira magumu."

Guterres asema yuko tayari kuanzisha mazungumzo kufufua uzalishaji wa kilimo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: VALENTYN OGIRENKO/REUTERS

Guterres ametahadharisha kuwa, vita vya Ukraine vinaongeza shinikizo zaidi kwa mataifa yanayoendelea. Ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba yuko tayari kuanzisha mazungumzo juu ya kufufua tena uzalishaji wa kilimo nchini Ukraine na kuongeza mgao wa chakula na mbolea katika soko la dunia licha ya vita vinavyoendelea.

Kwa mujibu wa vyanzo nchini Ukraine, takriban raia 200 bado wamekwama katika kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol. Vikosi vya Urusi viliahidi kusitisha mapigano kwa muda na kufungua njia salama za kuhamisha raia waliokwama katika maeneo ya vita jana Alhamisi, japo hakukuwa na habari zozote juu ya zoezi la kuhamisha raia hao.

Soma pia: Kansela Scholz wa Ujerumani asifu msaada wa Japan kwa Ukraine

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk amesema jaribio lengine la kuanzisha njia salama za kuhamisha raia limepangwa kufanika leo Ijumaa. Tangu Urusi ilipoivamia jirani yake Ukraine mnamo Februari 24 katika kile Moscow ilichokiita oparesheni maalum ya kijeshi, Marekani na washirika wake wa nchi za Magharibi wameiwekea vikwazo vikali Urusi.

Urusi yashtumu nchi za Magharibi kwa kuanzisha viya vya dunia vya kiuchumi

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia Picha: Carlo Allegri/REUTERS

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia, ameliambia baraza hilo kwamba nchi za Magharibi zinaendesha vita vya dunia vya kiuchumi dhidi ya Urusi na kwamba wanatumia fursa hiyo ya vita vya Ukraine kuikandamiza kiuchumi Urusi. Hata hivyo balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield ameishtumu Urusi kwa kulidanganya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Balozi huyo amesema Urusi ndiyo iliyoanzisha vita hivyo na kwamba nchi hiyo pekee ndiyo yenye uwezo wa kuvimaliza vita hivyo. Thomas-Greenfield ameitolea mwito Urusi kuweka chini silaha zake na kuondoa wanajeshi wake nchini Ukraine na kukumbatia diplomasia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksyy amesema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za matibabu na dawa katika maeneo ya mashariki na kusini yanayodhibitiwa na Urusi nchini Ukraine.

Soma pia: Kaburi jengine la pamoja lagunduliwa Mariupol

Zelenksyy amesema hakuna matibabu yanayowafikia wagonjwa hasa wa saratani na kwamba dawa za kupambana na maambukizi kutokana na bakteria pia ni chache. Amesema hali hiyo imewanyima fursa madaktari kuwahudumia wagonjwa au kuwafanyia upasuaji.

Katika hotuba yake ya kila siku kwa njia ya video, Rais huyo wa Ukraine ameongeza kuwa, wakati wa vita hivyo jeshi la Urusi limerusha makombora 2,014 katika ardhi ya Ukraine huku ndege za kivita za Urusi zilizorekodiwa katika anga ya Ukraine zikiwa 2,682.

Amesema miundombinu na majengo yaliyoharibiwa katika vita hivyo ikiwemo hospitali na vituo vyengine vya matibabu inakaribia 400.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW