1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Vikosi vya Urusi vinaendelea kuishambulia Kiev

29 Machi 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema vikosi vya Urusi bado vinaushambulia mji wa Kiev, licha ya kufurushwa nje ya Irpin, kitongoji cha kaskazini magharibi wa mji huo mkuu ambacho kimeshuhudia mapigano makali.

Ukraine-Krieg | Trümmer der jüngsten russischen Streiks in Kiew
Picha: Anastasia Vlasova/Getty Images

Akizungumza Jumatatu usiku, kiongozi huyo amesema Urusi bado inadhibiti vitongoji vya kaskazini na inajaribu kujipanga tena baada ya kuupoteza mji wa Irpin siku ya Jumatatu. Zelensky amewataka raia wa Ukraine wasiache kupigana katika vita hivyo.

Aidha, maafisa wa nchi hiyo wamesema makombora ya Urusi jana usiku yamelilenga ghala jengine la mafuta kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Kutokana na ving'ora vya uvamizi wa anga vinavyoendelea, wananchi walio jirani na eneo hilo wametakiwa kubaki kwenye makaazi yao.

Shambulizi la pili ghala la mafuta

Hilo ni shambulizi la pili na la hivi karibuni kuyalenga maeneo ya mafuta. Zelensky amesema mashambulizi hayo kwenye vituo vya mafuta yanalenga kuuvuruga msimu wa kupanda mazao Ukraine, nchi ambayo ni mlimaji mkubwa wa nafaka.

Aidha, Rais wa Marekani, Joe Biden amesema hatoomba radhi kutokana na kauli yake aliyoitoa kwamba Rais wa Urusi Vladmir Putin hawezi kuendelea kubakia madarakani, akifafanua kuwa matamshi hayo yalionesha ''ghadhabu yake ya kimadili'' na sio ''mabadiliko ya sera.'' Akizungumza Jumatatu na waandishi habari katika Ikulu ya Marekani, Biden amesema anataka kuweka wazi kwamba hatoi wito wa kuwepo mabadiliko ya sera na hivyo hatoomba radhi kutokana na kuelezea hisia zake binafsi, wakati akiwa ziarani mjini Warsaw, Poland.

Rais wa Marekani, Joe BidenPicha: Slawomir Kaminski/AGENCJA WYBORCZA via REUTERS

Biden amesema hana wasiwasi kwamba matamshi yake yatazidisha mvutano kuhusu vita vya Ukraine, kwani alikuwa akielezea hisia zake kuhusu Putin na kwamba tabia yake haikubaliki kabisa na sio kutaka mabadiliko. Biden amesema jambo la mwisho analotaka kuliona ni kujihusisha na vita vya ardhini au vita vya nyuklia na Urusi.

Wakati huo huo, nchi saba za Ulaya zimewataka wananchi wao kujizuia kujiunga na jeshi la Ukraine linalopambana na majeshi ya Urusi ambayo yameivamia nchi hiyo. Wito huo umetolewa na Mawaziri wa Sheria wa nchi za Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Uhispania, Italia, Luxembourg na Ubelgiji.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa baada ya mkutano wao uliofanyika Jumatatu mjini Brussels, mawaziri hao kwa kauli moja wamewakatisha tamaa wananchi wao kujiunga na makundi ya wapiganaji wa hiari wanaoelekea kwenye vita vya Ukraine.

Zelensky awaalika wageni kuisaidia Ukraine

Baada ya Urusi kuivamia kijeshi Ukraine Februari 24, Zelensky aliwaalika waziwazi wageni kwenda kuisaidia nchi yake kama sehemu ya jeshi la kimataifa ambalo lingepigana bega kwa bega na wanajeshi wa Ukraine.

Machi 6, Ukraine ilisema takriban watu 20,000 waliitikia wito huo. Akizungumza baada ya mazungumzo hayo na mawaziri wenzake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin alisema wanawakatisha tamaa watu kwenda kwenye eneo la vita. Amesema kwa ufahamu wake, watu wachache wameondoka Ufaransa ambao wanaweza kuthibitishwa.

Uingereza imesema kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner Group imepelekwa mashariki mwa Ukraine, ambako zaidi ya mamluki 1,000 huenda wakajiunga katika vita. Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Uingereza, mamluki hao wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa kundi hilo, wanatarajiwa kushiriki katika operesheni za kijeshi nchini Ukraine baada ya jeshi la Urusi kukumbana na upinzani mkali na kupata hasara kubwa.

Nembo ya kampuni ya Wagner GroupPicha: imageBROKER/Siegra Asmoel/imago images

Huku hayo yakijiri, mazungumzo ya siku mbili ya ana kwa ana yaliyopangwa kufanyika kati ya maafisa wa Ukraine na Urusi yanatarajiwa kuanza Jumanne mjini Istanbul, Uturuki. Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema atakutana kwa kikao kifupi na ujumbe wa Urusi na Ukraine kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo. Erdogan jana usiku ameliambia baraza lake la mawaziri kuwa mazungumzo ya simu aliyoyafanya kwa nyakati tofauti na Zelensky na Putin yanaendelea katika mwelekeo mzuri.

Hata hivyo, Erdogan hakutoa maelezo zaidi. Duru za awali za mazungumzo baina ya pande hizo yaliyofanyika kwa njia ya video na ana kwa ana yalishindwa kupiga hatua. Zelensky amesema mkutano wa ana kwa ana kati yake na Putin unaweza kuvimaliza vita vya Ukraine, ingawa mkutano wa aina hiyo kati ya viongozi hao wawili bado haujafanyika.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitri Peskov amesema Jumuia ya Kujihami ya NATO ni chombo cha kusababisha malumbano. Peskov amesema pia nchi yake itatumia silaha za nyuklia pale tu kutakapokuwa na kitisho dhidi ya taifa hilo, na sio kutokana na mzozo unaoendelea na Ukraine.

Waukraine 500,000 wamerejea tangu vita vilipoanza

Ama kwa upande mwingine, wananchi wapatao 500,000 wa Ukraine wamerejea kutoka nje tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi. Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa mpakani wa Ukraine Andriy Demchenko, wiki iliyopita pekee watu 110,000 walirejea nchini humo.

Siku ya Jumatatu Demcheko aliliambia gazeti la Ujerumani Die Welt kuwa wanane kati ya watu 10 waliorejea nchini humo ni wanaume. Amesema wengi wao wamerejea kutoka Poland. ''Takribani raia 352,000 wa Ukraine wameondoka Poland tangu vita vilipoanza,'' alisema Demcheko.

Kabla ya uvamizi wa Urusi, watu wapatao milioni 44 waliishi Ukraine. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, takribani watu milioni 3.9 wamekimbilia nje, huku milioni 2.3 wakiwa wamekimbilia kwenye nchi jirani ya Poland.

(ADP, AFP, AP, Reuters)