1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky: Wanajeshi 31,000 wa Ukraine wameuawa vitani

26 Februari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema zaidi ya wanajeshi 31,000 wamefariki vitani katika muda wa miaka miwili tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Ukraine | Volodymyr Zelenskiy na Oleksandr Syrsky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akizungumza na kamanda wa vikosi vya ardhini Oleksandr Syrsky wakati wa ziara katika mji uliokombolewa wa Izium.Picha: Ukrainian Presidential Press Off/ZUMAPRESS/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema ushindi wa nchi yake "unategemea" uungwaji mkono wa nchi za Magharibi.

Kiongozi huyo ameeleza matumaini yake kuwa Marekani itaidhinisha kifurushi cha msaada muhimu wa kijeshi kwa Ukraine.

Zelensky pia amekiri kuwa, wanajeshi 31,000 wa Ukraine wameuawa na kuongeza kwamba Urusi inapanga kufanya mashambulizi zaidi katika msimu ujao wa joto.

"Tutajiandaa kwa shambulio hilo. Mashambulizi yao walioyafanya tangu Oktoba 8 hayakuwa na matokeo yoyote, hilo naamini. Sisi kwa upande wetu, tutaweka mipango madhubuti na kuifuata," ameeleza Zelensky.

Ametoa wito kwa nchi za Magharibi kuiunga mkono Ukraine kwa dhati ili kuipa nafasi ya ushindi katika kumbukumbu ya miaka miwili ya uvamizi wa vikosi vya Urusi.

Soma pia: Stoltenberg: Ukraine na washirika "wasikate tamaa"

Katika wiki za hivi karibuni, wanajeshi wa Ukraine wamekabiliwa na uhaba wa risasi na makombora, baada ya mzozo katika bunge la Marekani kuhusu msaada wa kijeshi wa dola bilioni 60 kwa Kiev.

Wiki iliyopita, wanajeshi hao walilazimika kuondoka katika mji wa mashariki wa Avdiivka katika jimbo la Donestk ambako hali inaripotiwa kuwa mbaya.

Macron kuandaa mkutano kujadili kadhia ya Ukraine

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimkumbatia Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kabla ya mkutano katika Ikulu ya Elysee mjini Paris.Picha: Thibault Camus/AP/picture alliance

Wakati hayo yanaarifiwa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakuwa mwenyeji wa viongozi wa dunia mjini Paris kwa ajili ya mkutano wa kuimarisha uungwaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine.

Ofisi ya Macron imetangaza kuwa mkutano huo utawapa washiriki nafasi ya kuonyesha umoja pamoja na azma yao ya kuishinda Urusi.

Soma pia: Marekani yatangaza vikwazo vipya 500 dhidi ya Urusi

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Rais wa Poland Andrzej Duda, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte pamoja na viongozi wa mataifa ya ukanda wa Skandinavia na Baltic watakuwa miongoni mwa viongozi 20 watakaodhuria mkutano huo.

Marekani, Uingereza na Canada watatuma wanadiplomasia wa ngazi ya juu kwenye mkutano huo. Hata hivyo, hakuna wawakilishi kutoka India au China watakaohudhuria.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ataufungua mkutano huo kwa kutoa hotuba kwa njia ya vidio.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW