1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Watu 100,000 waondolewa miji ya Ukraine

11 Machi 2022

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema watu wapatao 100,000 wameondolewa kwenye miji ya nchi hiyo siku chache zilizopita kupitia njia za kiutu zilizokubaliwa.

Ukraine-Konflikt - Mariupol
Picha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/picture alliance

Akizungumza Ijumaa kwa njia ya video, Zelensky ameishutumu Urusi kwa kuzishambulia njia za kiutu na vituo ambavyo wanakusanyika watu waliokimbia Mariupol, huku akisema kuwa mji wa bandari wa Mariupol na mji wa karibu wa Volnovakha bado inazingirwa na majeshi ya Urusi. 

''Kwa kuzingatia kazi inayoendelea kwenye njia za kiutu, tayari tumewaondoa takribani watu laki moja siku mbili zilizopita. Mariupol na Volnovakha bado imezingirwa kabisa, ingawa tulifanya kila kitu muhimu kuhakikisha njia za kiutu zinafanikiwa, majeshi ya Urusi bado hayajasitisha mapigano. Licha ya hayo nimeamua kupeleka msafara wa malori yenye chakula, maji na dawa kwenda Mariupol,'' alifafanua Zelensky.

Kiongozi huyo pia ameishutumu Urusi kwa kufanya kila inaloweza kuwahadaa raia wa Ukraine kwenye miji iliyozingirwa na vikosi vya Urusi. Zelensky amewataka raia wenye mawasiliano na wakaazi wa Mariupol kuwaeleza wasikate tamaa ya kulipigania jimbo lao.

Zelensky pia amezungumzia madai ya Urusi kwamba Ukraine inatengeneza silaha za kemikali, akisema hakuna silaha za kemikali au silaha za maangamizi zinazotengenzwa Ukraine. Amesema ulimwengu mzima unajua hivyo.

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Instagram/@zelenskiy_official/via REUTERS

Huku hayo yakijiri, wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza kwamba Ijumaa itasitisha kwa muda mapigano ili kuruhusu kufungua njia kwa ajili ya kuwaondoa raia wa Ukraine kutoka kwenye miji ya Kyiv, Sumy, Kharkiv, Mariupol na Chernihiv. Yakiinukuu wizara hiyo, mashirika ya habari ya RIA na Interfax yamesema kuwa watu huenda wakasafiri kwenda Urusi au kwenye miji mingine ya Ukraine.

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema ana matumaini kwamba njia ya kiutu ya mji uliozingirwa wa Mariupol itafanikiwa kufunguliwa. Vereshchuk amesema mabasi yatapelekwa kwenye viunga vya Kyiv ili kuwachukua watu kwenye mji huo mkuu na kupeleka misaada kwa wale wanaobakia nyuma.

Umoja wa Mataifa kukutana Ijumaa

Ama kwa upande mwingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana Ijumaa kuzungumzia madai ya Urusi kwamba Marekani inatengeneza silaha za kemikali nchini Ukraine. Madai hayo yalitolewa mapema wiki hii na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, bila ya kuwepo ushahidi.

Marekani imejibu ikisema madai hayo ni ya uwongo na imeionya Urusi kwamba inaweza kuhalalisha kufanya mashambulizi ya silaha za kemikali. Aidha, Rais wa Marekani Joe Biden Ijumaa anatarajiwa kutoa wito wa kumaliza uhusiano wa kawaida wa biashara na Urusi.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema masharti ya kusitisha mapigano yaliyowekwa na Rais wa Urusi, Vladmir Putin hayakubaliki kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo. Kauli hiyo ameitoa baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na Putin pamoja na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz.

Eneo la kizuizi katika mkoa wa LutskPicha: Alexandra von Nahmen/DW

Wakati huo huo, wanajeshi wawili wa Ukraine wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Urusi kwenye kambi ya jeshi la anga ya Lutsk kaskazini magharibi mwa Ukraine. Mkuu wa mkoa wa Lutsk, Yuriy Pohuliayko amesema wanajeshi wengine sita wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea Ijumaa asubuhi.

Meya awataka wananchi wasichapishe picha

Meya wa Lutsk, Ihor Polishchuk aliandika katika ukurasa wake wa Facebook akisema mitipuko imetokea kwenye upande wa uwanja wa ndege na kuwataka watu wabakie ndani na kutochapisha picha zozote, anuani au viashiria vyovyote.

Takriban raia mmoja ameuawa katika mashambulizi ya Urusi kwenye eneo la Dnipro katikati mwa Ukraine. Mapema asubuhi Ijumaa mashambulizi matatu ya anga kwenye mji huo yameishambulia shule ya watoto wadogo, jengo la ghorofa moja na kiwanda cha viatu chenye ghorofa mbili.

Nao waasi wanaoiunga mkono Urusi ambao wanataka kujitenga wamechukua udhibiti wa mji wa Volnovakha, mashariki mwa Ukraine.

(DPA, AP, AFP, DW)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW