1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelenskyy asema vikosi vya Ukraine vimeukamata mji wa Urusi

15 Agosti 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema leo vikosi vya nchi yake vimechukua udhibiti kamili wa mji mdogo wa Sudzha uliopo kwenye mkoa wa mpakani wa Urusi wa Kursk ambao wanajeshi wa Ukraine waliuvamia wiki iliyopita.

Urusi | Mkoa wa Kursk| Ukraine
Kifaru cha jeshi la Ukraine kikiwa ndani ya ardhi ya Urusi.Picha: Anatoliy Zhdanov/Kommersant/Sipa USA/picture alliance

Tangazo hilo la Zelenskky limetolewa wakati Moscow imesema inapeleka wanajeshi wa nyongezakuvikabili vikosi vya Ukraine vilivyoingia ndani ya ardhi yake. 

Katika ujumbe alioutuma kupitia mitandao ya kijamii, Rais Zelenskyy amesema vikosi vya nchi yake vimepata mafanikio ya kuukamata kikamilifu mji wa Sudzha na kuwatimua wanajeshi wa Urusi waliokuwa wakiulinda.

Kiongozi huyo alipatiwa taarifa hizo na makamanda wa jeshi lake aliofanya nao mazungumzo leo mchana.

Amesema tayari vikosi vyake vinaanzisha kamandi ndogo ya kijeshi kwenye mji huo. Lakini hakutoa maelezo ya kina kuhusu kituo hicho wala kufafanua jukumu lake kwenye mji huo mdogo.

Mji wa Sudzha ambao ndiyo mkubwa zaidi kukamatwa na Ukraine ndani ya ardhi ya Urusi ulikuwa na wakaazi wasiozidi 5,000 kabla ya kuzuka kwa vita baina ya nchi hizo mbili mwaka 2022.

Ni katika mji huo ndio kunakutikana kituo kikubwa cha kupima gesi asilia ya Urusi inayosafirishwa kwa mabomba makubwa kupitia ardhi ya Ukraine kwenda mataifa mengi ya Ulaya.

Gesi husafirishwa kutoka kwenye visima vilivyopo huko Siberia na kisha hupitia hapo Sudzha na hatimaye kuingia kwenye miundombinu inayokatisha ardhi ya Ukraine.

Picha za satelaiti zaonesha uharibifu maeneo ya Urusi

Moto ukiwaka kwenye moja ya maeneo ya mji wa Sudzha.Picha: MIC Izvestia/IZ.RU/REUTERS

Ingawa taarifa za kudhibitiwa mji huo na vikosi vya Ukraine hazijaweza kuthibitishwa na vyanzo huru kutokana na vita vinavyoendelea, ikiwa madai hayo ni ya kweli basi itakuwa ni mafanikio makubwa ya jeshi la Ukraine ndani ya ardhi ya Urusi.

Kyiv iliwatuma wanajeshi wake kuvuka mpaka na kuingia Urusi kupitia mkoa wa mpakani wa Kursk mnamo wiki iliyopita.

Katika operesheni hiyo ya kustukiza na inayotajwa kuwa ya uthubutu usio na mfano, Ukraine inasema imefanikiwa kukamata ardhi ya Urusi yenye ukubwa wa kilometa 1,000 za mraba.

Picha za satelaiti zilizofanyiwa tathmini na shirika la habari la Associated Press zinaonesha athari za mashambulizi ya droni za Ukraine kwenye vituo kadhaa vya kijeshi vya Urusi kwenye mji wa Sudzha. 

Zinaonesha mahanga mawili kwenye uwanja wa ndege wa kambi ya kijeshi ya Borisoglebsk yameharibiwa na na kuna ishara pia ndege mbili za kivita zilizokuwa zimeegeshwa kwenye uwanja huo nazo zimelengwa.

Urusi yatangaza kupeleka wanajeshi zaidi kuulinda mpaka wake na Ukraine

Mapigano kati ya Ukraine na Urusi kwenye mkoa wa Urusi wa Kursk.Picha: Anatoliy Zhdanov/Kommersant/Sipa USA/picture alliance

Mapema hii leo gavana wa mkoa wa Kursk Alexei Smirnov aliamuru kuhamishwa kwa watu kwenye wilaya ya Glushkovo inayopatikana kilometa 45 kutoka mji wa Sudzha.

Uamuzi huo unaashiriavikosi vya Ukraine vinasonga mbele kuelekea wilaya hiyo.

Tangu mapema wiki hii mamia kwa maelfu ya warusi wamehamishwa kutoka kwenye mkoa huo wa mpakani kutokana na operesheni hiyo ya jeshi la Ukraine.

Hii leo pia waziri wa ulinzi wa Urusi alitangaza kwamba Moscow inapeleka wanajeshi zaidi kuulinda mkoa mwingine wa mpakani wa Belgorod.

Waziri Andrei Belousov amesema Urusi inachukua "hatua madhubiti" kuulinda mkoa huo dhidi ya mashambulizi ya Ukraine yanayofanywa na vikosi vilivyovuka mpaka.