Ziara ya Bi Clinton nchini Pakistan kumalizika leo.
30 Oktoba 2009Ziara ya kidiplomasia ya siku tatu ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, nchini Pakistan inamalizika leo. Ziara hiyo iligubikwa na mfululizo wa mashambulizi ya mabomu kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Taliban na wanamgambo wa al Qaeda.
Kabla ya kumalizika kwa ziara yake, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani, alipanga kukutana na viongozi wa kabila la Pashtun mjini Islamabad, kabila ambalo linadhibiti pande zote za mpaka wa Pakistan na Afghanistan, waandishi wa habari, pamoja na askari na wanasheria.
Bi Clinton alipanga kutumia ziara yake hiyo ya siku tatu katika eneo hilo lenye machafuko, kujaribu kuhamisha uungwaji mkono wa serikali ya kiraia, wakati ambapo jeshi la nchi hiyo likiendesha kampeni dhidi ya wapiganaji wa Taliban.
Lakini baada ya mikutano ya mara kwa mara, Bi Clinton alionekana kupoteza uvumilivu wakati wa mkutano wake na wahariri waandamizi na wafanyabiashara, na akawaambia kwamba magaidi wamekuwa wakiishi kwa usalama zaidi nchini Pakistan tangu mwaka 2002, na kwamba anashindwa kuamini kuwa hakuna mtu hata mmoja katika serikali ya nchi hiyo anayejua walipo magaidi hao, na hawawezi kupatikana kabisa, na akaongeza.
"Wanafanya mashambulizi zaidi ambayo ni ya kikatili na kuua watu wasiokuwa na hatia. Mnawaachia magaidi na wakereketwa wanakuwa wazuri wa kubomoa ingawa hawawezi kujenga. Hata hivyo, hapo ndipo tunapopata mwanya, kwa sababu leo waziri wa mambo ya nje na mimi tumejadiliana namna nchi mbili hizi zitakavyofanya kazi pamoja zaidi."
Amesema anadhani serikali ya nchi hiyo haijafanya juhudi za kutosha kuwatafuta magaidi hao, lakini dunia nzima inafahamu kwamba magaidi wanaishi nchini Pakistan.
Hakukuwa na taarifa yoyote iliyotolewa na serikali kuhusiana na maneno hayo ya Bi Clinton, lakini taarifa ya kijeshi iliyotolewa baada ya waziri huyo kufanya mkutano wa mkuu wa majeshi Ashfaq Kayani, ilisema tu kwamba mikutano hiyo ya kubadilishana uwezo ilikuwa na maslahi kwa pande zote mbili.
Baada ya ziara ya nchini Pakistan, waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani anatarajiwa kuelekea mashariki ya kati, ambapo atakutana na waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu, na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, katika kujaribu kushinikiza mpango wa amani.
Maafisa wa Marekani walio katika ziara ya Pakistan wamesema haijafahamika mapema bi Clinton atakutana na viongozi hao wapi, lakini wakati ni muafaka, kwa zingatio kuwa atakutana na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za kiarabu mapema wiki ijayo, nchini Morocco.
Msemaji wa waziri huyo P.J Crowly, amewaambia waandishi wa habari kwamba kwa sababu bi Clinton anaelekea katika ukanda huo, anaona ni fursa nzuri kufanya mashauriano ya moja kwa moja na viongozi hao pamoja na mawaziri wa nchi za kiarabu, katika kuimarisha juhudi za amani zinazoendelea.
Crowly amesema mkutano wa Morocco, ambao utafanyika pembezoni mwa mkutano wa maendeleo, utakuwa na umuhimu mkubwa katika kujenga uwezo wa mataifa ya kiarabu kushiriki katika harakati za amani mashariki ya kati.
Mwandishi:Lazaro Matalange/RTRE/AFP
Mhariri: Abdul-Rahman.