Ziara ya Bush Africa
16 Februari 2008DAR-ES SALAAM
Rais George W Bush wa Marekani anatazamiwa kuwasili nchini Tanzania muda wowote kutoka sasa katika zira yake ya siku sita barani Afrika ambayo itamfikisha pia nchini Ghana,Benin,Liberia na Rwanda.Akiwa safarini kuelekea Tanzani hapo jana rais huyo wa Marekani alisema mojawapo ya agenda zake ni kuzungumzia uwezekano wa kuhamisha kikosi cha wanajeshi wa Marekani kwa ajili ya Afrika kutoka Ujerumani na kukipeleka barani humo.Kiongozi huyo wa Marekani anatazamiwa kutafuta uungaji mkono wa viongozi wa Afrika juu ya wapi kuundwe makao makuu ya kikosi hicho kipya cha Marekani kwa ajili ya Afrika kinachojulikana kama AFIRICOM ambacho kitafanya kazi kwa ushirikiano na wanajeshi wa Africa.
Hata hivyo masuala mengine muhimu ambayo yanampeleka Bush barani Afrika ni pamoja na kuitangaza sera ya Marekani ya nchi za nje ,usaidizi kwa watu walioathirika na maradhi ya Ukimwi na Virusi vya HIV,pamoja na masuala ya kibiashara.Migogoro ya jimbo la Darfur nchini Sudan na Kenya pia yamo kwenye agenda ya rais Bush.Rais Bush hatazamiwi kufika Kenya lakini amemtuma waziri wake wa mambo ya nje Condolezza Rice kusafiri Kenya kusaidia kutafuta mwafaka wa suluhu ya kisiasa nchini humo.Hapo jana katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alimtolea mwito rais Bush kuzungumza na viongozi wa Africa juu ya kuwasaidia raia kuondokana na Umaskini pamoja na ukosefu wa mahitaji muhimu na Elimu.Wakati huohuo mamia ya watanzania waliandamana katika barabara za jiji la Daresalaam hapo jana kupinga ziara ya rais huyo wa Marekani wakibeba mabango yaliyokuwa na maandishi makali ya kumpinga.Usalama umeimarishwa katika mji huo.