1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Kansela Gerhard Schroader wa Ujerumani katika Jamhuri ya Umma wa Uchina na mkutano mkuu wa Chama kikuu cha upinzani, CDU, uliomalizika jana ndio masuala yaliozagaa katika uhariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani.

3 Desemba 2003
Kuyachambua magazeti hayo, huyu hapa Othman Miraji.

Kwanza tuanze na ziara ya Kansela Schroader huko Uchina. gazeti la KIELER NACHRICHTEN limeandika hivi:

+Mtu inafaa atafakari. Tena hasa kwa vile serekali ya Ujerumani ambayo hii leo bila ya kungoja hata kesho ingependa kuitoa nchi hii katika kutegemea nishati ya kinyukliya inataka kuwauzia Wachina kinu cha kinyukliya cha Hanau kwa bei rahisi sana. Na tena hasa nchi inayouziwa ni Uchina, dola inayozidi kupata nguvu katika eneo lenye umuhimu wa kijeshi na ambalo sio tulivu. Suali la kutafakari ni: jee nchi hiyo itapata kinu ambacho kitakuwa na nyenzo za kuweza kutengeneza mabomu ya atomiki? Ikiwa hiyo ndio njia mpya ya Ujerumani katika siasa yake ya kigeni, basi siasa hiyo inaweza tu kuzusha hofu na wasiwasi.+

Gazeti la FRANKFURTER RUNDCHAU lililipinga wazo hilo, likasema hivi:

+Kwa kupata teknolojia ya kinu cha Hanau, Uchina itaweza kutumia kiasi kikubwa cha Plutonium kutengenezea silaha za atomiki; na hilo ndio tatizo. Kwani, kama ilivyo madola mengine makubwa yalio na nishati ya kinyukliya, pia huko Uchina hakuna tafauti kubwa baina ya sekta inayotumia nishati ya kinyukliya kwa njia za kiraia na ile inayotumia kwa njia za kijeshi. Kujifanya kwamba unaweza kuiwekea Uchina kanuni za namna ya kukitumia kinu hicho cha kinyukliya ni kujaribu tu kufunika kombe ili mwanaharamu apite.+

Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf lilikuwa na wasiwasi juu ya pendekezo la Kansela Schroader kutaka kuviondosha vikwazo vya kuiuzia silaha Uchina. Lilikuwa na haya ya kusema:

+ Kuna msemo wa Kichina, nao ni kama hivi: Yule anayetaka kumpanda chuwi, basi afikirie kabla ya hapo mahala atakapoteremka kutoka mgongo wa chuwi huyo. Kwa Kansela wa Ujerumani ambaye amekuwa akivutiwa sana kuitembelea Uchina, yaonesha msemo huo bado ni mgeni kwake.Ama sivyo basi Gerhard Schroader asingetoa matamshi yake hayo kuhusu vikwazo vya silaha vilivowekwa na nchi za Ulaya dhidi ya Uchina, tena bila ya kujali na bila ya kutafakari.+

Kuhusu mkutano mkuu wa Chama cha upinzani cha CDU hapa Ujerumani uliofanyika Leipzig, gazeti la TAGESPIEGEL la Berlin liliandika kama hivi:

+Baada ya miaka ya mabishano baina ya viongozi wake, Chama cha CDU mara hii kimeweza kuwa kitu kimoja katika mkutano wake mkuu. Sasa kina kiongozi ambaye habishwi tena, na kimepitisha programu inayotia moyo. Chama hicho kimejivumbua upya kama chama cha mageuzi. Lengo la kiongozi wa chama hicho, Bibi Angela Merkel, ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2006, huenda hata mwaka 2005. Hadi wakati huo Bibi Merkel anahitaji wakati kuweza kuizidisha heba yake kama mtu anayetaka mageuzi.+

Vivyo hivyo liliandika gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG linalochapishwa Frankfurt an der Oder.

+ Angela Merkel ameipita mitihani kwa ushujaa. Hajawahi mwanamke huyo anayetokea Mashariki ya Ujerumani, kuwa bila ya kubishiwa kama ilivyo hivi sasa. Ikiwa hivi sasa ataweza kumpata mtetezi anayemtaka kutoka vyama vya CDU/CSU kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa Shirikisho, basi bibi huyo hatozuilika yeye mwenyewe kudai haki ya kuwa ni mtetezi wa Ukansela katika uchaguzi ujao.+

Gazeti la STTTGARTER ZEITUNG katika uhariri wake lilidai hivi: + Kwamba Chama cha CDU kimeunga mkono wazi wazi mapendekezo ya mkuu wake kwa wingi mkubwa na kimeifuata njia mpya na ya kijasiri ya Angela Merkel, hata kama ina hatari zake, yaonesha wazi wazi namna Merkel alivokuwa na nguvu ndani ya chama chake.+

Gazeti la Berlin ZEITUNG limeuchunguza umuhimu wa mkutano mkuu wa Chama cha CDU kwa serekali ya Ujerumani:

+Kwa Kansela matoeko ya mikutano mikuu yote miwili, ule wa chama chake cha SPD na wa chama cha CDU, sio ya kufurahisha. Hawezi sasa kupumua kwa kusema kwamba kama vile yalivo mabishano katika chama chake, pia yako mabishano makubwa zaidi ndani ya chama cha upinzani. Serekali ilio dhaifu na upinzani ulio na nguvu, hiyo ndio sura ya siasa ya Ujerumani mwishoni mwa majira ya mapukitiko ya mwaka 2003. Gerhard Schroader ana bahati kwamba kuna wakati mrefu sana hadi kufanyika uchaguzi mkuu ujao.+