Ziara ya Kansela Merkel barani Afrika Magazetini
12 Oktoba 2016Tuanzie lakini na njia panda inayoliunganisha bara la Afrika na Ujerumani. Gazeti la "Rhein-Necker" la mjini Heidelberg linaimulika ziara ya siku tatu ya kansela Merkel nchini Mali,Niger na Ethiopia na kuandika: "Hata wakati huu ambapo yuko bado madarakani nafasi ya Afrika katika ramani ya kidiplomasia ya serikali bado ni ndogo. Matatizo yanayotokea katika bara hilo hayazingatiwi. Mtu akizingatia ukweli kwamba kupunguzwa michango ya shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR,na Ujerumani ni miongoni mwa waliopunguza,ndio chanzo cha kufungwa kambi za wakimbizi nchini Jordan,basi hapo mtu hatokosa kutambua kwamba ziara ya Merkel barani Afrika si tukio la kukuzwa . Inatoa picha ya kurekebisha hali ya mambo na kuifanya iwe bora zaidi. Na hilo linastahiki sifa."
Kitisho cha kuselelea balaa la njaa duniani
Shirika la kimataifa la kupambana na njaa ulimwenguni limechapisha fahasara ya hali ya njaa ulimwenguni . Hali bado inatisha linaandika gazeti la "Märkische Oderzeitung la mjini Frankfurt /Oder. "Balaa la njaa linakawia kumalizika. Kwasababu ya vita na kwasababu serikali nyingi zimeoza kwa rushwa au hazifai kuwepo madarakni au yote hayo mawili. Lakini sababu kuu ni kwamba kuna ukosefu wa nia. Na hali hiyo inakutikana sio tu katika nchi nyingi zinazosumbuliwa na njaa bali pia katika nchi tajiri. Na ndio maana balaa la njaa halitotoweka ifikapo mwaka 2030. Dala bilioni 60 zinahitajika kwa mwaka ili kulifikia lengo hilo. Kiwango hicho ni sawa na asili mia 10 ya fedha zinazotolewa na Marekani kwaajili ya gharama za kijeshi. Kwa vyovyote vile lingekuwa jambo la maana kuwekeza upande huo na sio tu kwasababu zitapunguza maafa yanayosababishwa na njaa ulimwenguni,bali pia kwasababu zitawapatia matumaini watu wanaoishi katika maeneo masikini zaidi ya sayari yetu hii. Kupambana na njaa kutasaidia pia kulipatia jibu suala la wakimbizi.
Kasheshe ya Samsung Note 7
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na kasheshe ya kushika moto simu za mkononi chapa Note 7 za kampuni mashuhuri ya Korea ya Kusini Samsung. Gazeti la "Der neue Tag" la mjini Weiden linajiuliza:"Eti wakorea wenye tamaa wamezidiwa nini? Ndo kusema wanatanguliza mbele pupa badala ya usalama. Kwamba betri ya simu ya mkononi si kitu cha kuchezea kisichokuwa na hatari,hakuna asiyejua. Lakini mnunuzi anaamini bila ya shaka kwamba chombo alichokinunua hakitakuwa na hatari yoyote kwake. Pengine mashindano ya nani atakuwa wa mwanzo kutengeneza chombo chenye uwezo wa aina gani ndio chanzo cha kasheshe ya betri. Jee hayo ndio maendeleo ya ufundi usiokuwa na mipaka? Kishindo cha Samsung Note 7 ni onyo kwa sekta nzima ya mawasiliano ya kimambo leo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga