1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Papa Benedict nchini Marekani yafikia kilele

Mwakideu, Alex18 Aprili 2008

Benedict anatarajiwa kuhutubia baraza la Umoja wa Mataifa mjini New York

Papa Benedict wa kumi na sita akiwaaga waumini baada ya Misa iliyofanyika jana mjini WashingtonPicha: AP

Kinyume na desturi za kanisa katoliki Papa Benedict wa kumi na sita amekutana kwa mara ya kwanza na wahanga wa ubakaji walionyanyaswa kimapenzi na makasisi wa kanisa hilo.


Baadae Papa Benedict anatarajiwa kuhutubia kikao cha Umoja wa Mataifa mjini New York.


Ziara ya Papa Mtakatifu Benedict wa kumi na sita inaingia siku ya nne leo baada ya siku tatu zilizoshuhudia kiongozi huyo wa kanisa katoliki akikutana na kundi la wahanga wa ubakaji na kuwatia moyo.


Leo Benedict anatarajiwa kugusia maswala ya ulimwengu mzima; hii ikiwa ndio sababu kuu iliyompeleka nchini Marekani.


Kutoka mjini Washington Papa Benedict anatajiwa kuelekea mjini New York ambako atahutubia kikao cha Umoja wa Mataifa; hii ikiwa ni nafasi yake ya kwanza kuongea rasmi na ulimwengu mzima.


Mkutano huo utafuatia ule wa jana ambapo aliomba pamoja na wahanga wa ubakaji waliotendewa maovu hayo na makasisi wa kanisa hilo.


Duru kutoka vatican zinasema kwamba hotuba yake katika kikao cha Umoja wa Mataifa ndio itakayokuwa kilele cha ziara yake nchini Marekani.


Papa Benedict anatarajiwa kuzungumzia maswala ya haki za binadamu kabla ya kutembelea sinagogi moja mjini New York.


Kiongozi huyo wa kanisa katoliki aliwasili jumanne nchini Marekani kwa ziara ya siku sita ambayo kando na maswala mengine alikusudia kuitumia kulishughulikia swala la makasisi wa kanisa hilo walio katika visa vya ubakaji.


Baada ya kuhudhuria misa pamoja na waumini takriban 48 elfu mapema hapo jana, Papa Benedict alikutana na kundi dogo la watu waliobakwa na viongozi wa kanisa hilo. Pamoja aliomba na kundi hilo na kusikia matatizo wanayopitia.


Kwa huzuni alisema "Hakuna maneno ninayoweza kutumia kueleza uchungu na maumivu yanayotokana na dhuluma ya aina hii. Ni muhimu kwamba wale wale walioteseka wapewe mwongozo wa kiroho wa kina"


Kiongozi huyo aliwaahidi kuwaombea wahanga hao na jamii zao pamoja na wote wanaoteseka kutokana na ubakaji.


Papa Benedict tayari amesikika akiomba msamaha kuhusu visa hivyo akisema kwamba vinamtia aibu.


Kundi la wahanga waliodhulumiwa kimapenzi na makasisi lenye makao yake nchini Marekani Survivors Network of those Abused by Priests (SNAP) limefurahishwa na hatua hiyo ya Papa Mtakatifu lakini limesema kuna mengi ambayo yanahitaji kufanyika ili kulibadili kanisa na kuzuia visa vingine vya unyanyasaji wa kimapenzi.


Visa hivi vya vilianza kujitokeza baada ya askofu wa zamani wa Boston Kadinali Bernard Law kujiuzulu mwaka wa 2002 kufuatia malalamiko ya jinsi alivyokuwa akiwahudumia makasisi waliotajwa katikavisa vya unyanyasaji wa kimapenzi.


Kulingana na kikao cha maaskofu wa kanisa katoliki nchini Marekani mwaka jana kanisa hilo lilitoa msaada wa dola milioni 615 kwa ajili ya kumaliza kesi za unyanyasaji wa kimapenzi.


Benedict pia alikutana sirini na viongozi wa kiyahudi mjini Washington na kuwahimiza washirikiane na wakatoliki kuleta amani duniani.


Papa Benedict alikutana na Rais wa Marekani George Bish katika ikulu ya Rais na kumshawishi kutumia diplomasia kumaliza vita.


Hata hivyo hakugusia kuhusu vita vya Iraq isipokuwa aliongea kuhusu wakristo nchini humo.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW