Ziara ya Papa Benedikti nchini Lebanon
15 Septemba 2012Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Benedikti XV1, amewataka Wakristo na Waislamu katika Mashariki ya Kati kuunda jamii iliyostawi ya watu wa dini zote ambapo utu wa kila mtu na haki ya kuabudu kwa amani itahakikishwa. Papa alikuwa akizungumza na Viongozi wa kisiasa na kidini, katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu nchini Lebanon Jumamosi.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alisisitiza kwamba umma lazima ukatae ulipizaji kisasi, utambuwe makosa yake na kusameheana.
Maelfu ya watu wengi wao wakiwa Wakristo ikiwemo idadi kubwa ya watoto, walijipanga katika barabara inayoelekea kasri la Rais, asubuhi ya jua lililochomoza ili kumuona Papa Benedikti XV1 wakati akielekea Ikulu. Miongoni mwao walikuwemo Wamisri, Wairaki, Wajordan na Wapalestina, waliofika kujionea ziara yake ya kwanza nchini Lebanon tangu ile ya John Paul II mwaka 1997.
Papa Benedikti mwenye umri wa miaka 85 akitembea na gongo alikutana kwanza na Rais Michel Sleiman ambaye ni mkristo wa madhehebu ya Maronite. Baadae kabla ya kuwa na mazungumzo na viongozi wa Kiislamu alionana na na Waziri Mkuu Nagib Mikati, Muislamu wa madhehebu ya Sunni na Spika wa Bunge Nabih Berri,Mshia. Lebanon ina utaratibu wa kijadi ambapo nafasi tatu za Uongozi wa juu hutengwa kwa watu wa jamii hizo tatu za kidini. Pamoja na umati uliomlaki Kiongozi huyo kuwa mkubwa , ulinzi pia ulikuwa mkali.
Papa Benedikti alisema wale wanaowajibika kuishi kwa amani hawana budi pia kubadili nyoyo zao na ni pamoja na kukataa ulipizaji kisasi akiongeza kwamba amekuja na risala ya amani katika sehemu hii ya dunia na kwengineko Mashariki ya kati. Akauliza ,"kwanini Mwenyezi Mungu amezichagua ardhi hizi, na kwanini maisha ya wakaazi wake ni ya misukosuko ?
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani akajibu kwa kusema , anafikiri Mungu alizichagua ardhi hizo, ili ziwe ni mfano na ushahidi mbele ya dunia kwamba kila mwanamme au mwanamke anawajibu wa kujitolea kwa ajili ya amani na maridhiano. Moyo huo ni sehemu ya mpango wa Mwenyezi Mungu kuhusu roho na ameuweka ndani ya roho ya binaadamu.
Alisema amani inawezekana tu pakiweko na jamii iliyoungana yenye Umoja na kama tunataka amani basi hatuna budi kuyalinda maisha, alisema Papa Benedikti. Ratiba yake ya mwisho Jumamosi ni kukutana na vijana wa Lebanon Wakristo na wengineo, karibu na kijiji cha Bkerke. Papa Benedikti XV1 atarejea Roma kesho baada ya misa ya wazi mjini Beirut.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,afp
Mhariri: Mohamed Dahman