1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Pelosi Asia wagubikwa na usiri ikiwa atazuru Taiwan

1 Agosti 2022

Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amezuru nchini Singapore na kuzungumz na maafisa wa taifa hilo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya bara Asia huku wasiwasi ukitanda wa kutokea mvutano kama atazuru Taiwan.

Nancy Pelosi Asienreise | Singapur Premierminister Lee Hsien Loong
Picha: Mohd Fyrol/MCIAP/AP/picture alliance

Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi yuko nchini Singapore na amefanya mazungumzo na maafisa wa taifa hilo Jumatatu katika siku yake ya kwanza ya ziara anayoifanya katika kanda hiyo ya bara Asia. Hata hivyo swali ambalo limezidisha mvutano kati ya Marekani na China ni la uwezekano wa Pelosi kuzuru Taiwan na hilo bado ni kitendawili. 

Kulingana na wizara ya Mambo ya nje ya Singapore, Pelosi alikutana na Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong, Rais Halimah Yacob na mawaziri wengine.

Wizara hiyo imeeleza kwamba Lee aliukaribisha mshikamano wa muda mrefu wa Marekani na kanda hiyo. Pande zote mbili zilijadili njia za kuimarisha uhusianio wa kiuchumi kupitia miradi kama vile Mfumo wa Kiuchumi wa kanda ya Indo-Pasifiki.

Biden na Xi Jinping wakabiliana kwa simu

Lee na Pelosi pia walijadili vita nchini Ukraine, mvutano kuhusu Taiwan na China, na pia mabadiliko ya tabia nchi. Lee aliangazia umuhimu wa mahusiano thabiti kati ya Marekani na China kwa amani na usalama wa kanda hiyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa wikendi, Pelosi alisema atazuru Singapore, Malaysia, Korea Kusini na Japan kujadili biashara, janga la COVID-19, mabadiliko ya tabia nchi, usalama na utawala wa kidemokrasia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Zhao Lijian amekariri tahadhari za awali akisema kutakuwa na adhabu kali ikiwa Pelosi atazuru Taiwan.Picha: Liu Zheng/AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Hata hivyo Pelosi hakuthibitisha ikiwa atazuru Taiwan, kisiwa ambacho China inadai kuwa sehemu yake. Katika mazungumzo kwa njia ya simu wiki iliyopita, kati ya rais wa Marekani Joe Biden na rais wa China Xi Jinping, Jinping alitahadharisha dhidi ya Washington kuingilia masuala ya ndani ya kisiwa hicho.

Hakufafanua adhabu haswa, ila alisema wako tayari kwa lolote. "Jeshi la China halitazembea tu. China itachukua hatua thabiti kuulinda uhuru wake na mipaka yake.”

Pelosi anatarajiwa kuzuru Malaysia siku ya Jumanne.

Siku ya Alhamisi, Pelosi anatarajiwa kukutana na spika wa bunge la Korea Kusini Kimn Jin Pyo mjini Seoul kwa mazungumzo yatakayojikita kwenye masuala ya usalama wa kikanda, ushirikiano wa kiuchumi na mabadiliko ya tabia nchi.

Maswali yameibuka kuhusu uwekezano wa Pelosi kuzuru Taiwan suala ambalo linazusha mvutano kati ya Marekani na China. Picha: Allison Bailey/NurPhoto/picture alliance

Hakuna ratiba ambayo imetolewa kuhusu ziara yake siku ya Jumatano, wala hakuna taarifa kuhusu lini ataelekea Japan.

China inatizama uwezekano wa ziara rasmi ya Marekani kisiwani Taiwan kama njia ya kutilia uzito uhuru wa kisiwa hicho ambacho kwa miongo mingi kimekuwa kikijisimamia, lakini China inasisitiza kisiwa hicho ni sehemu yake. China yatishia hatua kali iwapo Taiwan itataka uhuru

China na Taiwan zilitengana 1949 baada ya wakomunisti kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Pande zote hukiri kuwa nchi moja lakini zinatofautiana kuhusu ni serikali gani inajukumu kuchukua uongozi wa kitaifa.

(AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW