1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Pompeo Ulaya na Mashariki ya kati yazua mshangao

14 Novemba 2020

Pompeo anawatembelea washirika waliokwisha anza kufungua ukurasa mpya bila ya Trump.

USA | Außenminister Mike Pompeo
Picha: AFP/M. Segar

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amewasili Paris Ufaransa leo Jumamosi, akianza ziara yake ya siku saba barani Ulaya na Mashariki ya kati. Ziara hii ya Pompeo hata hivyo inaonekana kama kitu kisichokuwa cha kawaida kutokana na kuwa takriban nchi zote alizopangiwa kuzitembelea zimeshampongeza Joe Biden kwa ushindi wake katika kiti cha urais wa Marekani. Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha na kuunga mkono vipaumbele vya rais anayeondoka madarakani Donald Trump.     

Pompeo atakwenda pia Mashariki ya kati, atakakotembelea makaazi ya Israel ya  walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, makaazi ambayo mawaziri wengine wa mambo ya nje wa Marekani waliomtangulia walijiepusha kuyatembelea.

Pompeo, Trump na chama cha Republican hawatambui ushindi wa Biden

Ikumbukwe kwamba hadi sasa mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani pamoja na rais wake na wanachama wengine wengi wa chama cha Republican hawajakubaliana na matokeo ya uchaguzi wa Marekani na hali hii ambayo sio ya kawaida huenda inaweza kuyagubika maswala jumla.

Picha: picture-alliance/dpa/K. Gideon

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian siku ya Ijumaa aligusia juu ya masuala magumu yaliyoko mezani kujadiliwa ikiwemo hali ya Iraq na Iran, ugaidi, Mashariki ya Kati pamoja na suala la China. Le Drian aliweka wazi kwamba kwa sasa Mike Pompeo ni waziri mwenzake wa mambo ya nje hadi Januari 20, tarehe ambayo kimsingi muhula wa rais Trump madarakani unafikia kikomo chake,na kwahivyo akabaini kwamba atampokea akifika Paris.

Mazungumzo  na Mike Pompeo yatafanyika Jumatatu kwa mujibu wa Le Drian ambapo pia ameeleza kwamba waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani atakutana pia na rais Emmanuel Macron. Rais huyo wa Ufaransa aliyezungumza kwa njia ya simu siku nne zilizopita na rais mteule wa Marekani Joe Biden  na kumpongeza, alikuwa na uhusiano wenye mashaka na Trump.

Viongozi wote wawili walionekana kutafuta ukaribu wa mwenzake, kwa mfano Macron alimfanya Trump kuwa mgeni wa heshima katika shughuli maarufu ya kitaifa ya gwaride la kijeshi la Ufaransa linalofanyika kila mwaka. Hata hivyo baade Trump aliojiondowa kwenye makubaliano ya kitaifa ya mazingira yaliyofikiwa Paris na hatua hiyo ilikuwa pigo kubwa kwa rais Macron.

Picha: Manuel Balce Ceneta/AP/picture-alliance

Waziri Pompeo baada ya kuondoka Ufaransa atakwenda Uturuki,Georgia,Israel,Umoja wa falme za kirabu, Qatar na Saudi Arabia na viongozi wa nchi zote hizo wameshampongeza wazi kabisa Joe Biden. Nchini Uturuki hakuna mkutano wowote uliopangwa hadi sasa kati ya Pompeo na kiongozi yoyote wa Uturuki.

Kando na Ufaransa,Uturuki,Georgia na Qatar zote zilikuwa na uhusiano wa mashaka na utawala wa Trump na haijawa wazi ikiwa Pompeo amepanga kushiriki kwenye shughuli zozote za wazi na viongozi hao au ikiwa atapokea maswali ya waandishi habari ambao hajawa na uhusiano mzuri sana nao.

Chanzo: (AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW