Jenerali Iliya Abbah kuongoza kikosi cha muungano
30 Julai 2015Msemaji mkuu wa jeshi la Nigeria Jenerali Chris Olukolade amesema Jenerali Iliya Abbah ambae awali aliongoza operesheni za kijeshi katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger-Delta, sasa ataongoza kikosi hicho kipya cha muungano wa kikanda.
Kikosi hicho cha wanajeshi 8,700 kinachounganisha nchi tano ambazo ni Nigeria, Niger, Chad, Cameroon na Benin, kinatarajiwa kufanikiwa kukomesha uasi wa zaidi ya miaka sita wa kundi hilo la Boko Haram ambao tayari umeshasababisha vifo vya takriban watu 15,000.
Buhari azuru Cameroon
Hayo yakijiri, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari hivi sasa yupo ziarani nchini Cameroon, kwa ajili ya mazungumzo juu ya namna ya kupambana na kuenea kwa tishio la kikanda la kundi la Boko Haram.
Msemaji huyo wa jeshi la Nigeria amesema kikosi hicho cha kikanda kinatarajiwa kuanza shughuli zake za mapambanao mapema iwezekanavyo, lakini hakuweka bayani siku gani kwa sababu za kimikakati.
Kundi la Boko Haram limeongeza kasi za mashambulizi, tangu Buhari kuapishwa kama rais mpya wa Nigeria mwezi Mei. Katika kipindi cha miezi miwili, kundi hilo limefanya wimbi la mashambulizi ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 800.
Kikosi hicho cha kikanda kitakuwa na makao yake katika makuu mji mkuu wa Chad N'Djamena, lakini bado hakuna maelezo zaidi juu ya shughuli zake. Jambo hilo limezuwa wasiwasi kwamba, huwenda kikosi hicho kikachelewa kuanza rasmi mashambulizi dhidi ya kundi hilo la uasi.
Rais Buhari amesema mazungumzo na rais Paul Biya ni moja wapo ya sehemu za juhudi zinazoendelea, za kujenga muungano wa kikanda wenye ufanisi zaidi dhidi ya kundi la Boko Haram.
Buhari tayari alishafanya ziara za kuzitembelea nchi za Chad na Niger, ambazo pia zimekumbwa na mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram. Rais huyo pia anatarajiwa kuitembelea nchi jirani ya Benin siku ya Jumamosi.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba