1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rais wa Iran nchini Iraq ni ya kuimarisha uhusiano

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
11 Machi 2019

Rais wa Iran Hassan Rouhani anaitembelea Iraq kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara. Ziara yake inatoa ishara kwamba Iran ina chaguo lingine kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.

Irak Staatsbesuch Hassan Rohani
Picha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Rais Hassan Rouhani amewasili katika nchi jirani ya Iraq leo hii Jumatatu kuanza ziara ya siku tatu nchini humo. Ziara hiyo ya kwanza rasmi ya Rouhani nchini Iraq inalenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Rais Rouhani atakutana na waziri mkuu wa Iraq Adil Abdul-Mahdi, Rais Barham Salih na huenda pia akafanya mazungumzo na washirika wa kishia ikiwa pamoja na aliyekuwa waziri mkuu Nouri al-Maliki na  kamanda wa vikosi vya Iraq vinavyoungwa mkono na Iran - PMU.

Rais wa Iran hassan Rouhani alipowasili nchini IraqPicha: hamshahrionline

Vyombo vya habari vya Iran pia vimesema huenda rais Rouhani akakutana na kiongozi mkuu Ayatollah Ali Sistan. Ziara ya Rouhani ni tofauti na ya Rais Donald Trump aliyefanya ziara fupi nchini Iraq wakati wa Krismas ambapo hakukutana na viongozi muhimu wa nchi hiyo, rais wa Iran, Rouhani anaongoza ujumbe mkubwa wa wanasiasa na wafanyabiashara.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javid Zarif hapo siku ya Jumapili alikutana na mwenzake wa Iraq mjini Baghdad, akizungumza baada ya mkutano wake na al-Hakim, Zarif aliishukuru Iraq kwa kuendeleza ushirikiano na nchi yake licha ya Marekani kuiwekea tena vikwazo. Zarif pia ameonyesha matumaini kwamba uhusiano kati ya nchi hizo jirani utaimarika zaidi.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran amesema ziara ya rais Rouhani nchini Iraq ina shabaha ya kutoa ishara madhubuti kwa Marekani kwamba sera yake ya kuishinikiza Iran kwa kiwango kikubwa kabisa, haitafua dafu wakati ambapo nchi hiyo inapanua mahusiano ya kiuchumi na kuonyesha ushawishi wake wa kisiasaa na kijeshi nchini Iraq.

Ziara hiyo inayoitwa ya kihistoria na mwanzo mpya katika uhusiano baina ya Iran na Iraq inafanyika wakati ambapo Iran inapambana na sera ya kutengwa kiuchumi baada ya utawala wa Donald Trump kuamua kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa nyuklia uliofikiwa mnamo mwaka 2015, na baada ya Marekani peke yake kuamua kuieweka nchi hiyo vikwazo.

vyanzo: p.dw.com/p/3Ek7h/DPA/AP

 

    

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW